Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipokea Ripoti ya Kamati
iliyoundwa na Serikali Kuchunguza Ajali ya Kivuko cha MV Nyerere kutoka kwa
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Mstafu,
Jenerali George Waitara, kwenye Makazi ya Waziri Mkuu jijini Dar es salaam,
Oktoba 25, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na wajumbe wa Kamati iliyoundwa na Serikali Kuchunguza Ajali ya Kivuko cha MV Nyerere baada ya kupokea Ripoti ya Kamati hiyo kwenye Makazi ya Waziri Mkuu jijini Dar es salaam, Oktoba 25, 2018. Kushoto ni Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu- Sera na Uratibu, Profesa Faustin Kamuzora na wapili kulia ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Mstaafu, Jenerali George Waitara.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amepokea ripoti ya
uchunguzi wa ajali ya kivuko cha MV Nyerere kutoka kwa kamati
iliyoundwa na Serikali kwa ajili ya kuchunguza ajali hiyo.
Amepokea ripoti hiyo
leo (Alhamisi, Oktoba 25, 2018) kutoka kwa Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mkuu wa Majeshi
ya Ulinzi Mstafu, Jenerali George Waitara,kwenye makazi ya Waziri Mkuu, jijini Dar es Salaam.
Waziri Mkuu ametumia
fursa hiyo kuishikuru kamati hiyo kwa niaba ya Rais Dkt. John Magufuli kwa kazi
kubwa waliyoifanya ambayo imethibitisha umakini wao.
Pia ameipongeza kamati
hiyo kwa namna walivyotumia muda wao vizuri kwa kufanya kazi hiyo na kutoa
mapendekezo kwa Serikali juu ya mambo waliyoyabaini.
“Nimepokea taarifa kwa
niaba ya Serikali, Serikali itafanya mapitio ya taarifa yote na viambatisho
vyake na itapitia kwa kina mapendekezo mliyoyatoa ambayo yote yatafanyiwa
kazi.”
Waziri Mkuu ameongeza
kuwa Serikali inaamini mambo yote yaliyosheheni katika taarifa hiyo ni yale
ambayo Watanzania wanasubiri kuona yakifanyiwa kazi.
MV Nyerere ilipindika
na kuzama Septemba 20, mwaka huu katika ziwa Victoria ambapo Watanzania zaidi
200 walipoteza maisha na wengine Zaidi ya 40 waliokolewa.
Septemba 24 mwaka huu Waziri Mkuu
alitangaza kamati ya kuchunguza ajali ya kivuko cha MV Nyerere yenye wajumbe
saba ambayo iliyoongozwa na Jenerali mstaafu, Waitara.
Akitangaza majina hayo kwenye kijiji cha
Bwisya katika kisiwa cha Ukara, wilayani Ukerewe, mkoani Mwanza, Waziri Mkuu
alisema wajumbe hao wanapaswa kuikamilisha kazi hiyo ndani ya mwezi mmoja.
Aliwataja wajumbe wengine ni aliyekuwa
Mbunge wa Ukerewe, Bw. Joseph Mkundi, Mhandisi Marcelina Magesa, Wakili Julius
Kalolo na Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Bi. Queen Mlozi.
Wengine ni SACP Camillus Wambura na
Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Uratibu Maafa katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Bw.
Bashiru Taratibu Hussein.
No comments:
Post a Comment