Monday, October 15, 2018

SERIKALI YAPIGA MARUFUKU UGAWAJI VIWANJA


Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Angeline Mabula akitoa
maelekezo kwa Kamishna Msaidizi wa Ardhi Kanda ya Simiyu Godwin Tumaini mara
baada ya kukagua majalada na mfumo wa ukusanyaji kodi ya ardhi katika halmashauri
ya walaya ya Rorya mkoani Mara.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Angeline Mabula
akikagua majalada katika ofisi ya ardhi katika halmashauri ya wilaya ya Rorya mkoa wa
Mara.
.......................................................................................................
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumbà na Maendeleo ya Makazi Angeline Mabula amepiga marufuku ugawaji viwanja ambayo tayari vimemilikishwa huku wamiliki wake wa awali wakitafutiwa eneo lingine.

Hatua hiyo inafutia kushamiri kwa  tabia iliyozueleka kwa baadhi ya watendaji wa sekta ya ardhi katika halmashauri kugawa maeneo ambayo tayari yana wamiliki wake kwa watu wengine wenye uwezo na baadaye kuwaahidi wamiliki halali kuwapatia kiwanja kingine.

Mhe Mabula alitoa kauli hiyo wilayani Musoma mkoa wa Mara mwishoni mwa wiki alipokutana na watendaji wa sekta ya ardhi katika Manispaa ya Musoma pamoja na halmashauri za wilaya za Musoma na Butiama wakati wa ziara yake ya kufuatilia utekelezaji wa maagizo yake aliyoyatoa wakati wa ziara yake ya februari mwaka 2018.

"Kuanzia sasa ni marufuku kwa watendaji wa sekta ya ardhi katika halmashauri kugawa viwanja 'pandikizi' katika maeneo ambayo tayari yameshamilikishwa kwa mananchi kwani suala hili limekuwa likileta migogoro mikubwa katika sekta ya ardhi" alisema Mabila.

Kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, suala hilo limekuwa likijitokeza sana hasa maeneo yanayovutia na mara nyingi linachangiwa na maafisa ardhi wasiokuwa waaminifu ambao humpatia mtu mwenye uwezo kiwanja kilichomilikishwa kwa ahadi ya kumpatia mmiliki halali kiwanja kingine.

Alisema,  serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Pombe Magufuli ambayo imekuwa ikiwatetea  watu wa hali ya chini haitavumilia hali hiyo iendelee kushamiri na kusema kuwa hatua kali zitachukuliwa kwa watendaji wote wa sekta ya ardhi watakaoendelea au kubainika kufanya mchezo huo.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Angeline Mabula ameshangazwa na kasi ndogo ya utoaji hati za ardhi kwa halmshauri ya wilaya ya Rorya ambapo jumlà ya hati 95 hazijapelekwa kwa Kamishna Msaidizi wa Ardhi Kanda ya Simiyu kwa ajili ya kukamilishwa tangu Oktoba mwaka 2017.

Kamishna Msaidizi wa Ardhi Kanda ya Simiyu Godwin Tumaini alieleza kuwa halmshauri hiyo imekuwa ukisusua katika kuwasilisha hati za ardhi katika ofisi yake kwa ajili ya kuakamilishwa ili kugawiwa kwa wananchi na kubainisha kuwa katika kipindi cha miezi mitatu ni hati moja tu ndiyo iliwasilishwa katoka ofisi yake halmashauri ya wilaya ya Rorya.

Kufuatia hali hiyo,  Mabula amemuagiza mkurugenzi wa halmashauri ya Rorya Charles Chacha kuwapangia maafisa ardhi watano wa halmshauri hiyo kila mmoja kushughulikia hati tano kwa wiki jambo litakalofanya halmshauri kutengeneza hati 35 kwa wiki.

Aidha,  Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi amewataka watendaji wa sekta ya ardhi kuwapa elimu wananchi wa Rorya kwa lengo la kupunguza migogoro ya ardhi ambayo mingi imechangiwa na uelewa mdogo  kwa wananchi pamoja na migogoro ya kikabila na koo.

"Cha msingi hapa ni kutoa elimu na siku nyingine mkienda kwa wananchi siyo kwa ajili ya kutatua tu migogoro bali iwe pia kutoa elimu na kuepuka masula ya siasa,  haiwezekani katika wilaya ya Rorya kila eneo linapotokea mgogoro wa ardhi basi lipelekwe jeshi hivyo elimu muhimu sana kwa wananchi" alisema Mabula.

Mmoja wa wakazi wa wilaya ya Rorya ambaye ni msaidizi wa mbunge wa Rorya Mzee Majwala ameiomba serikali kusaidia kutoa elimu kwa wananchi wa wilaya hiyo na kubainisha tatizo kubwa linaloikabili wilaya ya Rorya ni migogoro inayohusisha makabila na koo na kutolea mfano wa makabila ya Wasimbiti na Wajaluo ambapo alisema hata ukiitishwa mkutano wa usuluhishi katika makabila hayo wanakuja watu wachache. 

Mabula amemaliza ziara yake katika mkoa wa Mara baada ya kutembelea wilaya za Bunda, Serengeti, Rorya, Butiama na Musoma ambapo alifanikiwa kutatua migogoro ya mipaka baina ya vijiji na vijiji, kushughulikia kero za ardhi za muda katika maeneo hayo pamoja na kufuatia utekelezaji wa maagizo yake aliyoyatoa wakati wa ziara yake ya februari 2018.

No comments:

Post a Comment