Na Stella Kalinga, Simiyu
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.
Anthony Mtaka ametoa wito kwa wananchi mkoani humo na maeneo mengine nchini
kujitokeza kwa wingi kushirikia katika Maonesho ya Kitaifa ya Viwanda
Vidogo (SIDO), yatakayofanyika kuanzia Oktoba 23-28, mwaka huu katika Viwanja
vya Nyakabindi Bariadi mkoani humo na kubainisha kuwa Maandalizi yote
yamekamilika.
.Akizungumza na waandishi wa
habari Ofisini kwake Mtaka amesema Maonesho haya yatafunguliwa rasmi siku ya
Jumanne Oktoba 23, 2018 na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.
Kassim Majaliwa.
Ameongeza kuwa katika maonesho
hayo wajasiriamali, waoneshaji wa teknolojia mbalimbali wamealikwa na
kusisitiza kuwa hii ni fursa kwa wananchi wa Mkoa wa Simiyu na mikoa mingine
kuona ushindani katika uongezaji wa thamani wa mazao mbalimbali na fursa kwa
wajasiriamali kujifunza kutoka kwa wenzao.
“ Nitoe wito kwa wananchi wa
mkoa wa Simiyu kujitokeza kushiriki maonesho haya maana hii ni fursa kwao ya
kuweza kujielimisha katika maeneo mbalimbali ya teknolojia za viwanda hususani
viwanda vidogo, lakini pia wajasiriamali watapata nafasi ya kujifunza kutoka
kwa wenzao wa maeneo mengine nchini na nje ya nchi” alisema Mtaka.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi
wa Masoko na Uwekezaji wa Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO),
Shoma Kibende amesema tayari wajasiriamali kutoka mikoa mbalimbali
wamethibitisha kushiriki maonesho hayo na baadhi yao wameanza kuwasili.
“Wajasiriamali zaidi ya 1000
kutoka mikoa yote nchini wanatarajia kushiriki maonesho haya na baadhi yao
wameshaanza kuwasili, lakini pia kuna taasisi mbalimbali ambazo ni taasisi
shirikishi na SIDO, huduma za kupata ubora hii ni fursa pekee kwa Watanzania”
alisema.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya
ya Maswa, Mhe. Dkt. Seif Shekalaghe amesema zaidi ya wajasiriamali 51 kutoka
wilayani humo watashiriki katika kuonesha bidhaa mbalimbali ambazo
wametengeneza na kuzalisha kupitia viwanda vidogo.
Naye
Meneja wa SIDO Mkoa wa Kagera,Richard Mahela amesema maonesho ya SIDO ambayo ni
ya kwanza kufanyika Kitaifa yatawasaidia wajasiriamali kote nchini
kupanua masoko ya bidhaa zao kwa kuwa wameandaa vipeperushi vya bidhaa zao
ambavyo vitasambazwa kwa lengo la kusaidia kuwaunganisha na wanunuzi.
Maonesho
ya Viwanda Vidogo (SIDO) Kitaifa ambayo ni ya kwanza kufanyika ngazi ya Kitaifa
yatafunguliwa rasmi Jumanne Oktoba 23, 2018 na kuhitimishwa siku ya Jumapili
Oktoba 28, 2018 yakiwa na Kauli Mbiu: PAMOJA TUJENGE VIWANDA KUFIKIA
UCHUMI WA KATI”.
MWISHO
No comments:
Post a Comment