Friday, October 19, 2018

MAJALIWA AAGIZA WAHARIBIFU MIUNDOMBINU WAKAMATWE

 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza baada ya kukagua nyumba moja kati ya nyumba sita za walimu kwenye Shule ya Sekondari ya Mpalanga wilayani Bahi, Oktoba 19, 2019. Kushoto ni Mkuu wa wilaya ya Bahi, Mwanahamisi  Athumani. (Picha  na Ofisi ya Waziri Mkuu)
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikata utepe kuzindua  daraja la Chipanga wilayani Bahi, Oktoba 19, 2018. Wapili kushoto ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Selemani Jafo, Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhandisi Bilinith Mahenge, Wanne kushoto ni Mbunge wa Bahi,   Omary Badwel na wapili kulia ni Mkuu wa wilaya ya Bahi, Mwanahamisi Athumani. (Picha na ofisi ya Waziri Mkuu)
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizindua daraja la Chipanga wilayani Bahi, Oktoba 19, 2018.  Kushoto ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za mikoa na Serikali za Mitaa, Selemani Jafo na wapili kushoto ni Mbunge wa Bahi,   Omary Badwel. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  akipata maelezo kutoka kwa Mganga Mkuu wa Kituo cha Afya cha Bahi, Kassim Kolowa  (kushoto) kuhusu vifaa vilivyopo kwenye chumba cha upasuaji cha Kituo hicho  wakati alipokitembelea, Oktoba 19, 2018. Wapili kulia ni Mkuu wa wilaya ya Bahi, Mwanahamisi Athumani. (Picha na ofisi ya Waziri Mkuu)
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na  Bibi Subi Mchome, ambaye ni mmoja wa wazazi waliojifungua salama katika wodi ya wazazi ya Kituo cha Afya cha Bahi  mkoani Dodoma, Oktoba 19, 2018. Wapili kushoto ni Mganga Mkuu wa Kituo hicho, Kassim Kolowa.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Mtalaam wa Maabara, Petronila Olomi  (kushoto) wakati alipotembealea Maabara ya Kituo cha Afya cha Bahi mkoani Dodoma, Oktoba 19, 2018. Kulia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) , Selemani Jafo na Wapili kushoto ni Mganga Mkuu wa Kituo hicho, Kassim  Kolowa. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)



            ..................................................................................................
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amezindua daraja la Chipanga na kuagiza waharibifu wa miundombinu  ya barabara kukamatwa na kufikishwa mahakamani ili kudhibiti tabia iliyoibuka ya baadhi ya watu kung'oa alama za barabarani.

Majaliwa ametoa agizo hilo leo wilayani Bahi wakati akizindua daraja la Chipanga wilayani Bahi akiwa ziarani wilaya humo akikagua miradi mbalimbali ya Maendeleo.

Amesema kumekuwa na tabia  ya watu wasiokuwa waaminifu ya kuharibu miundombinu ya barabara na kingo za madaraja tabia jambo ambalo linapaswa kukemewa.

Amewataka wananchi kila mmoja kuwa mlinzi mwenzake lakini pia Jamii ya eneo hilo kuunda vikundi vya ulinzi ili viweze kuwakamata wahalifu hao wa miundombinu ya barabara na madaraja na kuwafikisha mahakamani.

"Kumeibuka tabia ya watu wachache wasiokuwa na nia njema,wanang'oa alama za barabarani na kingo za madaraja ,vitendo hivi vinasababisha ajali,hao ni watu wasiopenda Maendeleo  watolewe taarifa,wakamatwe ,wafikishwe mahakamani na tutawafunga." Amesema Majaliwa

Awali akikagua ujenzi wa nyumba ya walimu yenye uwezo wa kuishi walimu sita katika shule ya sekondari Mpalanga, Majaliwa amepongeza ujenzi wa nyumba hiyo na kuahidi kuwa serikali itaendelea kutatua kero zinazowakabili walimu huku akiagiza wilaya hiyo kujenga shule ya msingi kila Kijiji.

 Akimkaribisha kuzindua daraja hilo,  Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais,Tawala za  Mikoa na Serikali za Mitaa Selemani Jafo amesema,tayari Serikali imetoa sh. billioni 2.18 kwa ajili ya ujenzi wa daraja hilo na mkandarasi tayari ameshalipwa Sh.Bilioni 2.14.

Amesema,kabla ya ujenzi wa daraja hilo,kulikuwa na athari nyingi kwa wananchi ikiwemo kukata mawasiliano baina ya wananchi wa upande mmoja na Halmashauri yao ya wilaya ya Bahi na hivyo kukosa huduma muhimu waliokuwa wakizihitaji ikiwemo watoto kushindwa kwenda shule.

Aidha amesema,awali wakati wa ujenzi unaanza alikabiliana na changamoto mbalimbali ikiwemo mkandarasi  kushindwa kuendana na kasi iliyotakiwa lakini baadaye walienda sawa na hatimaye daraja limezinduliwa.

Kadhalika, amesema serikali imetoa Sh.Bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa vituo Vya Afya vitatu Vya Wilaya hiyo na Sh.Bilioni 1.5 zitapelekwa Mwaka huu wa fedha kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya wilaya.

No comments:

Post a Comment