Waziri wa kilimo Mhandisi Dkt Charles Tizeba (Mb) akitangaza zuio la Halmashauri kutoa vibali vya kununua kahawa wakati akihutubia maelfu ya wanachi waliojitokeza kwenye mkutano wa hadhara uwanja wa Changarawe Wilayani Karagwe kwenye muendelezo wa ziara ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Kassim Majaliwa (Mb) aliyoianza Jana tarehe 6 Octoba 2018 mkoani Kagera. (Picha Na Mathis Canal-WK)
Na Mathias Canal-WK,
Karagwe-Kagera
Waziri wa kilimo Mhandisi Dkt Charles Tizeba (Mb)
amezuia Halmashauri zote nchini kujihusisha na utoaji wa vibali kwa wafanyabiashara
vya kununua kahawa kwa wakulima.
Dkt Tizeba ametoa zuio hilo Leo tarehe 7 Octoba 2018
wakati akihutubia maelfu ya wanachi waliojitokeza kwenye mkutano wa hadhara
uwanja wa Changarawe Wilayani Karagwe wakati wa muendelezo wa ziara ya Waziri
Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Kassim Majaliwa (Mb) aliyoianza
Jana tarehe 6 Octoba 2018 mkoani Kagera.
"Wafanyabiashara wa kahawa ili wanunue zao hilo
walikuwa wanaenda kuomba kibali cha ununuzi kilichokuwa kinatolewa na
Halmashauri za wilaya, Hili jambo tumelitafakari na wenzangu wa Wizara hususani
watendaji pamoja na Bodi ya kahawa tumeona halina maana tena" Alikaririwa
Dkt Tizeba
Waziri Tizeba alisema kuwa Wafanyabiashara hawana
sababu ya kuomba vibali kwenye Halmashauri vya kununua kahawa badala yake
itatosha kuwa na leseni ya biashara ya Kahawa inayotolewa na Bodi ya Kahawa
Tanzania, jambo ambalo linawatambulisha wafanyabiashara kwamba wanalipa kodi.
"Sasa hivi tunaingia kwenye mfumo wa ushirika
hivyo Wafanyabiashara watanunua kahawa kupitia mfumo huo mahususi hivyo hakuna
sababu ya kusumbuliwa na Halmashauri kwa kupewa vibali" Alisisitiza
Aidha, Kuhusu kahawa ya madaraja ya chini, Waziri
Tizeba alisema kuwa kahawa hiyo kwa kipindi kirefu imekuwa ikizuiliwa kuuzwa
nje ya nchi. Hivyo kwa mujibu wa utafiti wa kubaini namna inavyotumika nchini
ilibainika kuwa kahawa hiyo inanunuliwa na watu wachache ambao ndio wanaratibu
utaratibu wa kuuza nje huku waliokoboa wakizuiwa kuuza nje.
"Jambo hili sio sawa, sisi tunachotaka wakulima
washiriki kwenye mnyororo wa thamani utakaowafanya wawe na uwezo wa kutafuta
mnunuzi nchini au nje ya nchi watakapopewa bei nzuri" Alisema
Dkt Tizeba aliongeza kuwa Kahawa hiyo itauzwa popote
Duniani kutegemea na kiasi cha fedha kitakachokuwa rafiki na chenye tija kwa
mkulima.
MWISHO.
No comments:
Post a Comment