Wednesday, October 17, 2018

DKT TIZEBA ATOA SIKU MBILI KWA MRAJISI WA USHIRIKA MKOANI MBEYA KUSAJILI VIKUNDI VYOTE VINAVYOZALISHA KOKOA

Waziri wa Kilimo Mhandisi Dkt Charles Tizeba (Mb) akihutubia mamia ya wananchi waliojitokeza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji na Kata ya Mwaya Wilayani Kyela akiwa katika ziara ya kikazi ya siku moja kufuatilia changamoto za uuzaji wa zao hilo, Leo Octoba 17, 2018. (Picha Zote Na Mathias Canal, WK)
Sehemu ya wananchi waliojitokeza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji na Kata ya Mwaya Wilayani Kyela Waziri wa Kilimo Mhandisi Dkt Charles Tizeba (Mb) Leo Octoba 17, 2018.
Waziri wa Kilimo Mhandisi Dkt Charles Tizeba (Mb) akikagua jinsi Kokoa inavyohifadhiwa mara baada ya kutembelea ghala kuu la kuhifadhia Kokoa Wilayani Kyela (KYECU) akiwa katika ziara ya kikazi ya siku moja kufuatilia changamoto za uuzaji wa zao hilo, Leo Octoba 17, 2018.
Waziri wa Kilimo Mhandisi Dkt Charles Tizeba (Mb) akihutubia mamia ya wananchi waliojitokeza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji na Kata ya Mwaya Wilayani Kyela akiwa katika ziara ya kikazi ya siku moja kufuatilia changamoto za uuzaji wa zao hilo, Leo Octoba 17, 2018.

Na Mathias Canal-WK, Tunduma-Mbeya

Waziri wa Kilimo Mhandisi Dkt Charles Tizeba (Mb), amemuagiza Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Mbeya Bi Angela Maganga kuhakikisha kuwa vikundi vinavyozalisha kokoa hai vinasajiliwa kwenye vyama vya ushirika ili kutopoteza soko lao maalumu Ulaya.

Waziri Tizeba ametoa agizo hilo leo Jumatano Octoba 17, 2018 wakati akihutubia mamia ya wananchi waliojitokeza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji na Kata ya Mwaya Wilayani Kyela akiwa katika ziara ya kikazi ya siku moja kufuatilia changamoto za uuzaji wa zao hilo.

Agizo hilo linajili wakati ambapo ushirika umezidi kuwanufaisha wakulima wengi nchini hususani katika mazao makuu ya biashara ya Tumbaku na Korosho ambapo Dkt Tizeba ametoa siku mbili kuanzia leo Jumatano Octoba 17, 2018 hadi siku ya ijumaa Octoba 19, 2018 vikundi vya ununuzi wa kokoa kuwa vimesajiliwa.

Alisema kuwa mfumo wa stakabadhi ghalani utakuwa ni mkombozi pekee kwa wakulima wadogo na wa kati kwa kuwawezesha kupata bei nzuri ya mazao yao, ukilinganisha na bei zilizokuwa zinatolewa na wafanyabiashara wanaponunua mazao yakiwa shambani kwa kutumia vipimo ambavyo sio sahihi.

Alisisitiza kuwa wakulima wamekuwa wakipunjwa bei ya mazao na wafanyabiashara hivyo kupitia mfumo wa ushirika wakulima watakuwa na fursa ya kupanga bei pasina kunyonywa na wafanyabiashara hao.

Alitaja kuwa ushirika ni dhana ya kuleta maendeleo kwa kushirikiana, Dhana hiyo imefanikiwa kuleta mabadiliko ya kiuchumi na kijamii katika kipindi cha miaka kadhaa iliyopita ambapo uanzishwaji wa vyama vingi vya ushirika kwa sasa unatokana na elimu watu wengi waliyoipata kuhusu Ushirika. “Ni wazi kuwa katika kipindi cha miaka miwili hivi, imani kwa vyama vya ushirika imeongezeka na vyama vingi vinaendelea kuundwa hasa vile vya kuweka na kukopa, yaani SACCOS” Alikaririwa Dkt Tizeba

Sambamba na agizo hilo pia, Waziri wa kilimo amemtaka Kaimu Mrajisi huyo wa vyama vya ushirika mkoa wa Mbeya kusimamia uchaguzi wa viongozi wa vyama vya msingi vya ushirika katika Wilaya ya Kyela kwani kumekuwa na malalamiko ya muda mrefu ya wakulima wa kokoa kutokuwa na imani na viongozi waliopo madarakani.

Kokoa ni zao la biashara ambalo linalimwa na kustawi katika Wilaya ya Kyela na baadhi ya maeneo ndani ya Halmashauri ya Busokelo wilayani Rungwe mkoani Mbeya Matunda ya zao hili yanatumika katika kutengeneza bidhaa mbalimbali ikiwemo kinywaji cha kuchangamsha kama majani ya chai, chokuleti nk.

Miaka ya nyuma zao hili halikuwa na thamani kwa wakulima wa wilaya hizo wala kwa jamii, ambapo kabla ya miaka ya 1999, wakulima walikuwa wakilima zao hilo kwa mazoea kutokana na kukosa soko la uhakika, ambapo hivi sasa serikali imeweka mkazo katika usimamizi wa zao hilo.

MWISHO.

No comments:

Post a Comment