Sunday, October 21, 2018

DKT TIZEBA APOKEA KWA MASIKITIKO MAKUBWA TAARIFA ZA VIFO VYA WATUMISHI WATANO

Na Mathias Canal-WK, Buchosa-Mwanza

Waziri wa kilimo Mhandisi Dkt Charles Tizeba amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya vifo vya watumishi watano wa wizara ya kilimo waliofariki kwa ajali ya gari wakiwa safarini kutokea Dodoma kuelekea Mwanza kikazi.

Waziri Tizeba amepokea taarifa hizo akiwa katika ziara ya kijimbo ya ukaguzi wa utekelezaji wa ahadi zake jimboni alizozitoa wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu mwaka 2015.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Mhandisi Mathew Mtigumwe kwa waandishi wa habari imeeleza kuwa Watumishi hao waliopatwa na mauti ni Stella Joram Ossano (39), Esta Tadayo Mutatembwa (36), Abdallah Selemani Mushumbusi (53), Charles Josephat Somi na Erasto Mhina (43).

Waziri Tizeba anatoa pole kwa familia, ndugu, Jamaa, Marafiki na watumishi wote wa Wizara ya kilimo kwa kupoteza nguvu kazi ya Taifa tena watumishi hao wakiwa safari kutekeleza majukumu ya kiserikali.

Amewasihi wanafamilia na wananchi wote kwa ujumla kuwa wavumilivu na wastahimilivu katika kipindi hiki kigumu cha majonzi ya kuondokewa na wapendwa wao.

Kufuatia msiba huo mkubwa kwa wizara ya kilimo, Waziri wa kilimo Mhandisi Dkt Tizeba amelazimika kukatisha ziara yake ya siku nne jimboni Buchosa ili kuungana na watumishi na familia za marehemu kuomboleza msiba huo.

Mwenyezi Mungu azipumzishe roho za marehemu mahala pema peponi. Amina

MWISHO.

No comments:

Post a Comment