Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), Vumilia Zikankuba
Na Mathias Canal, NFRA-Dodoma
IKIWA msimu wa kununua mazao
umeanza, Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula
(NFRA), Vumilia Zikankuba amewataka wakulima kuhakikisha wanazingatia
ubora wa mahindi.
Aidha, amesema nchi inachakula
cha kutosha na kusisitiza kuwa katika msimu wa kwanza wa ununuzi wa mahindi bei
ya NFRA ni wastani wa Sh 380 hadi Sh 400 kwa kilo.
Akizungumza na waandishi wa
habari ofisini kwake Mjini Dodoma, Zikankuba alisema NFRA haitaweza kununua
mahindi mabovu na kusisitiza wakulima kuwa na mahindi yenye ubora ambayo
yatawasaidia kupata masoko ya nje pia.
" Haiwezekani NFRA itumia
fedha za Serikali kununua mahindi yasiyokidhi viwango vya ubora na machafu
kutoka kwa wakulima. Hivyo wakulima wanapaswa kuzalisha mahindi kwa kuzingatia
viwango vya ubora vinavyokidhi vigezo vya soko..
Aliongeza: “Lazima chakula
tunachonunua kizingatie ubora. Tunataka tubadilishe taswira ya NFRA kwa sababu
awali kulikuwa na tatizo la chakula kuharibika kwa kipindi kifupi.”
Zikankuba alisema ili
kuhakikisha mahindi ya wakulima yanaweza kukidhi viwango vinavyotakiwa NFRA
tayari imekwishatoa elimu kwa wakulima kupitia vikundi na kwenye vyombo vya
habari.
Alibainisha kuwa baada ya elimu
hiyo wakala umefanikiwa ambapo wakulima kutoka maeneo ya Makambako, Sumbawanga na
Mpanda wameanza kuzalisha na kuuza mahindi yenye ubora kwa NFRA.
“Changamoto iliyopo ni kwa
baadhi ya wakulima wachache ambao bado wamekuwa wagumu kubadilika na wale ambao
wanaamini wakitumia nafasi zao wanaweza kuuza mahindi yasiyo na ubora,"
Alisema kwa mkulima kuwa na
mahindi yenye ubora unatoakiwa utasaidia katika kupata soko la NFRA, pia katika
taasisi zingine zinazonunua nafaka hiyo za ndani na nje ya nchi.
"Dhima ya serikali ni
kwenda uchumi wa kati kupitia uchumi wa viwanda, kwa mahindi pekee hayatumiki
kwa chakula pekee, bali kutengeneza bidhaa mbalimbali. Hivyo hatuwezi kufikia
Tanzania ya viwanda endapo wakulima watazalisha malighafi zisizokuwa na ubora,”
alieleza.
Viwango vinavyopaswa kuzingatiwa
na wakulima wa mahindi ni kwamba unyevunyevu usizidi asilimia 13.5, takataka
asilimia 0.5 na punje zilizovunjika zisizidi kwa asilimia 2.
Viwango vingine ni punje
zilizoliwa na wadudu na zilizosinyaa zisizidi asilimia moja, punje mbovu
asilimia mbili na punje za rangi tofauti zisizidi asilimia 0.5.
Zikankuba alitoa msisitizo kwa
wakulima kutunza chakula badala ya kukiuza chote.
“Msimamo wa Rais (John Maguful)
wa kutotoa chakula cha msaada upo sahihi kwa sababu kuna maeneo walikwishazoea
kupelekewa chakula cha msaada. Msimamo huo umelenga kuwahamasisha wananchi
kutunza chakula, haya malalamiko ya hatuna chakula yanachangiwa na uzembe wa
wananchi wa kuuza chakula chote,” Vumilia, alibainisha.
Alisema jukumu la wakala ni
kutunza chakula kwa ajili ya dharura kama kumetokea majanga kama mafuriko,
njaa, tetemeko na majanga mengine ambayo wanachi watahitaji msaada wa
chakula.
Kuhusu bei ya mahindi ambayo
NFRA imeanza kununua mahindi kwa wakulima Zikankuba alisema ni wastani wa Sh
380 kwa kilo hadi Sh 400 kwa kilo kulingana na eneo na eneo, na ni bei
inayoendana na mwenendo wa bei ya soko.
“ Mfano bei ya soko ya
mahindi mkoani Ruvuma ni Sh 250 kwa kilo, lakini sisi kama NFRA tunanunua kwa
bei ya juu ya kuanzia Sh 350 hadi 380 kwa kilo," alisema.
Aliongeza: “Mkoani Dodoma
NFRA inanunua Sh 420 kwa kilo, Makambako Sh 400, Shinyanga Sh 500, Katavi
na Ruvuma Sh 350 hadi 380. Bei hiyo bado ni ya juu ukilinganisha na bei ya soko
iliyopo,” alifafanua.
Aidha, Zikankuba alisema ziada
ya mazao yote yaliyozalishwa na wakulima msimu huu imefikia tani milioni 2 huku
ziada ya mahindi pekee ni tani 970,000.
Zikankuba alisema NFRA
imetengewa Sh bilioni 15 kwa ajili ya kununua tani 28,000 kwa awamu ya kwanza
ikiwa ni asilimia 2 ya ziada ya mahindi iliyopo.
Zikankuba alisisitiza kuwa NFRA
inazingatia ubora wakati wa kununua kwa kuwa ni haki na muhitaji kupatiwa
chakula bora na Salama kwa afya wakati wa dharula hivyo mahindi ambayo
hayana ubora yakituzwa kwa muda mrefu ghalani yanakuwa na nafasi kubwa kupata
vimelea vya fangasi ambao husababisha uwepo wa sumu kuvu katika nafaka
hiyo.
Alisema kuwa Sumu kuvu ni hatari
sana kwa afya ya mlaji. Tatizo hili kwa kiasi kikubwa sana, linaweza kuepukika
kwa mkulima kufuata mbinu bora za kilimo, mbinu bora za utayarishaji nafaka na
mbinu bora za kuhifadhi nafaka baada ya kuvuna. Lengo la NFRA ni kutoa chakula
chenye ubora na salama wakati wa dharula.
MWISHO
No comments:
Post a Comment