Monday, August 6, 2018

WAUGUZI WAOMBWA KUTOA TAARIFA ZA WALENGWA WA TASAF

Wauguzi wa hospitali ya wilaya ya Nyamagana jijini Mwanza wameombwa kutoa ushirikiano katika kujaza taarifa sahihi za walengwa wa mpango wa kunusuru kaya masikini TASAF.

Kauli hiyo imetolewa na afisa ufuatiliaji wa mpango wa kunusuru kaya masikini TASAF jijini Mwanza, Ndugu Samson Kagwe wakati akizungumza na wauguzi wa hospitali hiyo ambapo amewataka kuhakikisha wanawasajili walengwa hao katika daftari maalumu mara tu wanapofika kituoni hapo kwaajili ya kupata huduma  pamoja na  kujaza fomu maalumu za mpango  na kadi za kliniki kwa lengo la kupata taarifa sahihi zitakazotumika na serikali kwaajili ya utekelezaji wa mipango mbalimbali ya kimaendeleo yenye nia ya kupunguza umasikini kwa wananchi wake

‘… Tunawaomba nyie kama wadau wenzetu muweze kutusaidia kutoa taarifa za hawa walengwa, Na hili ndilo jukumu letu kubwa ambalo tunalo la kujaza rejista maalumu lakini pia kuwatolea taarifa katika ile fomu ya TASAF …’ Alisema

Aidha Ndugu Kagwe amewataka wauguzi hao kuzingatia muda wa uwasilishaji wa fomu hizo sambamba na kuwaeleza athari za kutojaza taarifa sahihi za walengwa  ikiwemo ukatwaji wa ruzuku kwa kaya ambayo itashindwa kuwasilisha taarifa zake za uhudhuriaji wa kliniki kwa mwezi husika.

Kwa upande wake moja ya wauguzi waliouhudhuria kikao kazi hicho Bi. Wada mbali na kumshukuru afisa huyo wa TASAF kwa kuendesha kikao kazi cha mafunzo ya namna ya kujaza fomu za mpango wa kunusuru kaya masikini, ametaja faida mbalimbali alizozipata kupitia kikao hicho ikiwemo kujua uhusiano wa huduma za afya na elimu kwa mama na mtoto wa chini ya umri wa miaka mitano ambao ni wanufaika wakubwa wa mpango wa kunusuru kaya masikini TASAF huku akiahidi kutoa ushirikiano katika kutimiza lengo la serikali la kupambana na umasikini nchini.

No comments:

Post a Comment