Monday, July 9, 2018

WAZIRI WA KILIMO DKT TIZEBA ATEMBELEA KITUO CHA UNUNUZI WA PAMBA- CHATO

Na Mathias Canal-WK, Chato-Geita

Waziri wa Kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba  leo 9 Julai 2018 amekagua zoezi la ukusanyaji na ununuzi wa Pamba katika Kijiji cha Mlimani kilichopo katika Kata ya Muungano Wilaya ya Chato Mkoani Geita.

Akizungumza na uongozi wa Chama cha ushirika cha Rubambangwe wakati wa ununuzi wa Pamba Mhe Tizeba amepiga marufuku kwa wakulima kuitoa Pamba yao kwa mnunuzi (kampuni) bila malipo yaani kwa mkopo hivyo kuagiza zoezi hilo la ununuzi kusimama mpaka hapo fedha za kununua zitakapopatikana.

"Sisi kama serikali hatuwezi kukubali hata kidogo wakulima wetu kuendelea kukopwa kwani kufanya hivyo ni kufifihisha na kutothaminiwa juhudi na nguvu za mkulima jambo ambalo linarudisha nyuma chachu na fursa ya Maendeleo ya Kilimo cha Pamba" alikaririwa Mhe Tizeba

Alisema kuwa lengo la serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli katika utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi ni kuwanufaisha wakulima kupitia sekta ya Kilimo si vinginevyo.

Dkt Tizeba alitembelea Chama Cha Ushirika Rubambangwe akiwa Safarini kuelekea Mkoani Kagera kwa ziara ya siku tatu kwa ajili ya muendelezo wa utekelezaji wa agizo la Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli aliyeagiza Wizara ya Kilimo kufatilia kwanini wakulima wa zao la Kahawa wanauza Kahawa nchini Uganda sambamba na kujua kwanini wakulima wamecheleweshewa malipo yao.

Akiwa Mkoani Kagera Waziri Tizeba atakutana na viongozi wa Mkoa wa Kagera, kukutana na vyama vya msingi (AMCOS), Wadau wa zao la Kahawa ili kujadili na kujionea mwenendo wa soko la zao hilo.

MWISHO.

3 comments:

  1. Safi sana kiongoz. Hakika atairudisha pamba kwenye hadhi yake

    ReplyDelete
  2. Hali hii ya kuwakopa wakulima ikiendelea kushamili itawavunja nguvu wakulima wa zao hili la pamba

    ReplyDelete