Na
Mwandishi Wetu
KAMATI
ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, imeitaka serikali kufanya tathmini ya
viwanja vya ndege nchini, inavyojiendesha kwa faida na hasara, ili iweze
kuvihudumia vyema.
Makamu
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Hawa Mchafu ametoa kauli hiyo hivi karibuni
wakati kamati hiyo ilipofanya ziara kwenye Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha
Julius Nyerere (JNIA), na kupata taarifa mbalimbali za uendeshaji.
Mhe.
Hawa amesema tathmini hiyo itasaidia kupunguza viwanja ambavyo ni mzigo kwa
kuwa havizalishi ipasavyo na kuwa tegemezi kwa vingine.
“Serikali
ifanye tathmini upya ya viwanja vya ndege ili iweze kuangalia vile
vinavyozalisha na kuviwekea mkazo hata ikiwezekana ivigawe kwa kanda,” amesema
Mhe. Hawa.
Hata
hivyo awali katika taarifa yake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya
Ndege Tanzania (TAA), Bw. Richard Mayongela ameiambia Kamati hiyo kuwa moja ya
changamoto TAA inakutana nayo ni pamoja na kujiendesha kwa taabu kutokana na kuhudumia
viwanja vingi visivyozalisha na kuwa tegemezi kwa vingine vichache
vinavyozalisha.
Bw.
Mayongela amesema kati ya viwanja vyote 58 vya ndege vingi ni tegemezi kwa
zaidi ya asilimia 90, ambapo mapato mengi yanatoka kwenye Kiwanja cha Ndege cha
Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) na viwanja vichache vinavyozalisha.
Amesema
changamoto nyingine ni uchakavu wa miundombinu ya viwanja, maegesho ya ndege na
ufinyu wa majengo ya abiria katika viwanja vya ndege vya Dodoma, Mwanza, Mafia,
Arusha na Ziwa Manyara; kutokuwa na mfumo wa kuongozea ndege wakati wa kutua na
kuruka, ambapo husababisha viwanja vingi kutumika kwa saa 12 pekee kwa
kushindwa kutua nyakati za usiku.
“Tatizo
jingine ni uchakavu wa magari ya zimamoto na uokoaji yaliyopo kwenye baadhi ya
viwanja, hivyo kunahatarisha usalama wa abiria na ndege; hali kadhalika wapo
wananhi wanaovamia maeneo ya viwanja nao husababisha tutumie gharama kubwa za
kuwaondoa,” amesema Bw. Mayongela.
Hata
hivyo, Bw. Mayonbgela amesema pamoja na TAA kukabiliwa na changamoto la
kutokuwepo kwa uzio kwa baadhi ya viwanja vya ndege, sasa wapo mbioni kujenga
uzio kwenye Kiwanja cha Ndege cha Mwanza, ambapo itasaidia kupunguza wananchi
na mifugo kukatiza kwenye barabara ya kutua na kuruka kwa ndege.
Akizungumzia
suala la uvamizi Mweyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Suleiman Kakoso amewataka
wananchi kuacha kuvamia maeneo ya viwanja vya ndege ambavyo yapo halali
kisheria.
“Viwanja
vyote ni vya serikali na hao wanaovamia wanaonekana, basi waondolewe kulingana
na sheria kwani wapo kwenye mikoa ambayo viwanja vipo,” amesema Mhe. Kakoso.
Kwa
upande wake Naibu Waziri wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya
Ujenzi), Mhe. Elius Kwandikwa amesema TAA inafanya jitihada ya kununua magari
ya zimamoto na kuboresha miundombinu mbalimbali ili kuviweka viwanja vyake
katika hali bora.
MWISHO.
No comments:
Post a Comment