Naibu Waziri wa Madini Mhe Doto Mashaka Biteko
Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Profesa Shukran Manya akiwasilisha taarifa ya uchunguzi wa shughuli za uchimbaji madini ya kinywe na vito katika machimbo ya Epanko mbele ya Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko, Mkuu wa Wilaya ya Ulanga, Jackob Kassema pamoja na watendaji kutoka Wizara ya Madini (hawapo pichani) kwenye ofisi ya Mkuu wa wilaya UlangaKutoka kulia ni Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko, Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Profesa Shukran Manya na Kamishna wa Madini kutoka Tume ya Madini Dkt. Athanas Macheyeki wakielekea kwenye machimbo ya Epanko yaliyopo katika wilaya ya Ulanga mkoani Morogoro
Na George Binagi, Morogoro
Naibu Waziri wa Madini Mhe Doto
Mashaka Biteko ameagiza kusitishwa shughuli za uchimbaji madini katika machimbo
ya Epanko iliyopo eneo la Mahenge katika Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga mkoani
Morogoro kutokana na machimbo hayo kukiuka kanuni na sheria za uendeshaji.
Naibu Waziri Biteko ametoa agizo
hilo leo 10 Julai 2018 ametoa agizo hilo kufuatia ripoti ya timu maalumu
aliyoiunda mwezi uliopita na Kamishina wa Madini nchini kuonyesha hakuna
usimamizi na udhibiti mzuri wa madini ya vito aina ya Spinel, Green-Gernel
pamoja na Ruby katika machimbo hayo na hivyo kuikosesha serikali mapato.
Mhe.Biteko
ametoa muda wa siku tatu shughuli zote katika machimbo hayo ziwe zimesitishwa
hadi pale taratibu zote za kisheria zitakapofuatwa ikiwemo wamiliki wote
kuilipa serikali hasara itakayobainika kutokana na biashara ya madini hayo
kufanyika kiholela huku akiongeza kwamba serikali inakusudia kuanzisha Ofisi ya
Madini katika wilaya ya Ulanga itakayosimamia kwa karibu mwenendo wa shughuli
za uchimbaji madini katika wilaya hiyo.
Ameagiza Kamati ya Ulinzi na
Usalama ikiongozwa na Mkuu wa Wilaya Ulanga Mhe Jacob Kassema kuhakikisha
hakuna kampuni inayoondoa mitambo yake katika eneo la Epanko kutokana na baadhi
ya wachimbaji kutaka kuondoka eneo hilo kinyemela baada ya kubainika walikuwa
wakifanya shughuli zao bila kufuata taratibu ikiwemo kutokuwa na leseni za
uchimbaji.
Naye Katibu Mtendaji wa Tume ya
Madini nchini, Profesa Shukrani Manya amesema baadhi ya wamiliki wa migodi
katika machimbo ya Epanko wamekiuka taratibu kulingana na leseni za uchimbaji
madini jambo ambalo serikali haiwezi kulivumilia na hivyo kuwataka wachimbaji
wote kuhakikisha wanafuata taratibu zilizowekwa ili kufanya shughuli zao
kihalali na kwamba watakaoshindwa kufanya hivyo watanyang’anywa leseni zao.
Mmoja wa wamiliki wa mgodi
katika eneo la Epanko, Salim Hasham ambaye pia ni Mkurugenzi wa kampuni ya Ruby
International amesema wako tayari kufuata taratibu zote huku akiiomba serikali
kuwaruhusu kuendelea na shughuli za uchimbaji.
Itakumbukwa kwamba mwezi
uliopita Naibu Waziri Biteko alifanya ziara katika machimbo ya Eponka na
kubaini mapungufu kadhaa ikiwemo malalamiko kutoka kwa wananchi wa Kijiji cha
Eponka wanaolalamika kudhulumiwa stahiki zao, utiririshaji ovyo wa maji taka
katika mkondo wa mto Kilombero pamoja na uwepo wa usimamizi mbovu wa madini na
hivyo kuisababishia serikali hasara kutokana na ukwepaji wa kodi na utoroshaji
madini, hivyo Naibu waziri huyo wa madini kuagiza iundwe tume maalum ili
kuchunguza uendeshaji wa biashara katika machimbo hayo.
Katika kutekeleza agizo hilo,
Katibu Mtendaji Tume ya Madini nchini Profesa Shukurani Manya aliteua timu ya
wataalamu sita ikiongozwa na Mwenyekiti Profesa Justinian Ikingura kutoka Chuo
Kikuu cha Dar es salaam ili kufanya ukaguzi maalumu katika maeneo ya uchimbaji
madini ya vito ikiwemo Spinel, Green-Gernel pamoja na Ruby na mradi tarajiwa wa
madini ya Kinywe (Graphite) ambapo ripoti hiyo imeonyesha ukiukwaji wa taratibu
za uchimbaji na biashara ya madini hayo.
MWISHO.
No comments:
Post a Comment