Na George Binagi-GB Pazzo, BMG
Naibu Waziri wa Madini Mhe Doto Mashaka
Biteko amewaagiza Maafisa Madini nchini kuhakikisha wanatenga maeneo kwa ajili
ya wachimbaji wadogo, badala ya kutoa kipaumbele kwa wachimbaji wakubwa pekee.
Biteko amesema serikali itaendelea
kuwatufia leseni ya uchimbaji watu wote waliohodhi maeneo makubwa yenye madini
bila kuyaendeleza ili wachimbaji wadogo wapatiwe maeneo hayo.
Naibu Waziri huyo aliyasema hayo Julai 17,
2018 wakati akizungumza na wachimbaji wadogo katika wilaya ya Mbinga mkoani
Ruvuma, kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Masugulu.
“Ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi
ukurasa wa 35 tamko namba 25 imetuelekeza tukawatengee maeneo ya kuchimba
wachimbaji wadogo, Na mimi nimekuja kuwapa taarifa kwamba mtu yeyote kwenye
Wizara ya Madini asiyefuata utaratibu huo hataki kazi yake”. Alikaririwa na
kuongeza;
“Ninachukua nafasi hii kuwaagiza Maafisa
Madini wote nchini wakiwemo wa Songea, wasikilizeni wachimbaji wadogo, marufuku
kumuona tajiri wa maana kuliko masikini. Hawa tukiwasimamia vizuri, matajiri
watatoka humu humu”. Alisisitiza Biteko.
Awali Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji
na Wafanyabiashara wa Madini mkoani Ruvuma (RUVREMA), Ndg Isack Ngerangera
alimpongeza Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli
kwa kuchukua hatua stahiki ili kulinda rasilimali madini nchini ikiwemo kufanya
marekebisho ya sheria ya madini.
Ngerangera alisema wachimbaji wadogo
mkoani Ruvuma wanaamini baadhi ya changamoto zinazowakabili ikiwemo ukosefu wa
maeneo ya uchimbaji zitatatuliwa ambapo aliomba wapewe baadhi ya maeneo ambayo
yamekaliwa na watu wenye leseni ambazo hawazifanyii kazi na hivyo kuikosesha
serikali mapato.
Naye Mkuu wa Mkoa Ruvuma Mhe Christina
Mndeme alisema serikali itaendelea kupima maeneo kwa ajili ya shughuli
mbalimbali ikiwemo uchimbaji madini, ufugaji pamoja na kilimo na hivyo kuwataka
wananchi kuheshimu maeneo hayo kwa kufanya shughuli zao bila kuingiliana ili
kuepuka migogoro isiyo ya lazima.
Naibu Waziri wa Madini Mhe.Dotto Biteko
akizungumza na wachimbaji wadogo wa madini katika Kijiji cha Masugulu wilaya ya
Mbinga mkoani Ruvuma
Wachimbaji wadogo wilayani Mbinga
wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa Ruvuma Mhe Christina Mndeme baada ya Naibu Waziri wa
Madini Mhe.Doto Biteko kukutana na wachimbaji hao akiwa ziarani mkoani humo
Mmoja wa wananchi akinasa ujio wa Naibu
Waziri wa Madini katika Kijiji cha Masugulu wilayani Mbinga
No comments:
Post a Comment