Sunday, July 22, 2018

MHANDISI MTIGUMWE AITAKA TARI KUBORESHA MFUMO WA UTAFITI WA KILIMO NCHINI

Katibu Mkuu Wa Wizara ya kilimo Mhandisi Mathew Mtigumwe akizungumza jambo Jana 21 Julai 2018 wakati akitoa maelezo ya Wizara ya kilimo kabla ya kumkaribisha Mgeni rasmi-Waziri wa kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba kuzungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa Bodi ya taasisi ya Utafiti wa kilimo Tanzania iliyofanyika kwenye viwanja vya ofisi ya TARI-SERIAN Jijini Arusha.
Waziri wa kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba akikata utepe kuzindua Bodi ya Taasisi ya Utafiti wa kilimo Tanzania iliyofanyika TARI-SERIAN Jijini Arusha jana tarehe 21 Julai 2018. Wengine ni Mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi TARI, Dkt Yohana Budeba (Katikati) na Katibu Mkuu wa Wizara ya kilimo Mhandisi Mathew Mtigumwe.
Katibu Mkuu Wa Wizara ya kilimo Mhandisi Mathew Mtigumwe akizungumza jambo Jana 21 Julai 2018 wakati akitoa maelezo ya Wizara ya kilimo kabla ya kumkaribisha Mgeni rasmi-Waziri wa kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba kuzungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa Bodi ya taasisi ya Utafiti wa kilimo Tanzania iliyofanyika kwenye viwanja vya ofisi ya TARI-SERIAN Jijini Arusha.
Baadhi ya watafiti kutoka vituo mbalimbali vya utafiti Tanzania-TARI wakifatilia kwa makini hafla hiyo.

Na Mathias Canal, Arusha

Katibu Mkuu Wa Wizara ya kilimo Mhandisi Mathew Mtigumwe ameitaka Taasisi ya utafiti Wa kilimo Tanzania-TARI kuboresha mfumo wa utafiti wa kilimo hapa nchini na kuhakikisha kuwa matokeo ya tafiti hizo yanajibu hoja za wanachi.

Katibu Mkuu huyo ameyasema hayo Jana 22 Julai 2018 wakati akitoa maelezo ya Wizara ya kilimo kabla ya kumkaribisha Mgeni rasmi-Waziri wa kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba kuzungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa Bodi ya taasisi ya Utafiti wa kilimo Tanzania iliyofanyika kwenye viwanja vya ofisi ya TARI-SERIAN Jijini Arusha.

Mhandisi Mtigumwe alisema kuwa utafiti ni muhimu katika uendelezaji wa sekta ya kilimo hususani kwa kuzingatia changamoto za kilimo zinazoendelea kuibuka kila siku.

Alisema nchi nyingi katika ukanda wa mashariki na kusini kwa Afrika zimeanzisha taasisi zao za utafiti ili kumrahisishia mkulima kuongeza tija katika kilimo ikiwa ni pamoja na kupata elimu juu ya mbinu bora za kilimo, kutumia kwa ufasaha mbolea za kupandia na kukuzia pamoja na kufuata Njia za kisasa wakati wa kupanda.

Mtigumwe aliongeza kuwa katika ukanda huu wa Afrika Mashariki nchi ya Tanzania ilikuwa nchi ya kwanza kuanzisha chombo hicho na wakati huo kilikuwa kinaitwa Tanzania Agricultural Research Organisation-TARO na Tanzania Livestock Research Organisation-TARILO ambapo baada Taasisi hizo zilivunjwa na kuwa idara ya utafiti wa Maendeleo katika Wizara. "Baada ya uhitaji kuongezeka ambapo mtazamo ni kuepuka yaliyotokea nyuma rasmi imeanzishwa TARI kwa ajili ya ufanisi zaidi" Alikaririwa Mhandisi Mtigumwe

Aidha, Mtigumwe amempongeza Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli kwa kuridhia kuanzishwa kwa Taasisi hiyo muhimu ya utafiti wa kilimo ambayo itachangia kupatikana kwa mabadiliko chanya katika sekta ya kilimo kwani mchakato wa kuanzisha TARI ulianza tangu mwaka 2010 na hatimaye kupata sheria ya kuanzishwa Taasisi ya utafiti wa kilimo tarehe 30 Septemba 2016.

Alisema  Taasisi hiyo imekuja wakati muafaka ambapo serikali ya awamu ya tano imekusudia kwa kauli moja kufikia uchumi wa viwanda hivyo ili kuchagiza juhudi hizo za serikali ya awamu ya tano Wizara ya kilimo imekusudia kuchagiza uanzishwaji wa viwanda nchini kwa kuimarishwa uzalishaji kwenye sekta ya kilimo.

Awali, Mkurugenzi wa Taasisi ya utafiti wa kilimo Tanzania-TARI Dkt Geofrey Mkamilo aliitaja Dira ya TARI kuwa ni kuwa taasisi mahiri ya utafiti wa kilimo nchini Tanzania na Kimataifa huku dhima yake ikiwa ni kugundua na kuhimiza matumizi ya teknolojia mbalimbali za kilimo ili kuongeza tija, uhakika wa chakula na lishe, kuwa na kilimo endelevu na chenye mchango chanya katika ukuaji wa uchumi wa nchi kwa kushirikiana na wadau wa kilimo wa Kitaifa na Kimataifa kwa ujumla.

Alisema TARI imekusudia kuweka mfumo mahsusi wa utafiti utakaowezesha ugunduzi, uzalishaji, upatikanaji na usambazaji wa teknolojia sahihi za kilimo nchini na kujenga uwezo wa wataalamu na miundombinu ya utafiti.

MWISHO

No comments:

Post a Comment