Thursday, July 26, 2018

MD KAYOMBO: TATIZO LA MAJI KUWA HISTORIA UBUNGO

Na Mwandishi Wetu, Dar es salaam

Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo ndugu John Lipesi Kayombo ameapa kutatua tatizo la ukosefu wa maji katika manispaa hiyo ambalo limekua kero kubwa kwa wananchi.

Akitembelea ujenzi wa miradi mbalimbali ya visima vya maji ili kujiridhisha na ujenzi huo ikiwa ni sehemu ya kutekeleza ilani ya Chama Cha Mapinduzi, Mkurugenzi huyo amewataka wahandisi hao kuongeza kasi katika utendaji wao pamoja na kuvijenga visima hivyo kwa ubora maana ni fedha za wananchi na mwisho wa siku wamalize kwa wakati ili wananchi waweze kupata maji hayo kwa haraka.

“Labda niwatake nyie wakandarasi serikali tunachokitaka ni thamani ya fedha tunayolipa iende sambamba na mradi, msije mkajenga na kumaliza alafu hii zege hapa ikaja ikaanguka. Mwisho wa siku wananchi wanaiamini serikali na wanataka watumie maji haya” alisisitiza mkurugenzi Kayombo

Miradi hiyo aliyotembelea ndugu Kayombo ni pamoja na mradi wa ujenzi wa kisima cha kusambaza maji mtaa wa Matosa Kata ya Goba na maeneo jirani ambao unagharimu shilingi milioni 99,072,564/=, pia alitembelea na kukagua ujenzi wa mradi wa kisima cha kusambaza maji Mbezi Makabe chenye uwezo wa kuhifadhi lita 9000 za maji na kuhudumia wakazi zaidi ya 70,000 na gharama yake ni shilingi milioni 611,447,675/=, na mwisho mkurugenzi alitembelea mradi wa ujenzi wa kisima cha maji kata ya King’azi wenye thamani ya shilingi milioni 53,770,320, na kujiridhisha na kuwataka waongeze kasi zaidi.

Aidha Mwenyekiti wa kamati ya maji Kata ya King’azi ndugu Aidani Mlowe ameishukuru sana serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt John Pombe Magufuli kwa utendaji wake kwa wananchi hasa baada ya mradi huo wa maji kufika katika kata hiyo.

“Hapa King’azi ilikuwa ni shida ambayo haielezeki yaani akina mama walikua wanakewnda kukesha visimani usiku kucha, hata wahamiaji walikuwa angalabu mtu kuja kuhamia huku ni shida akiangalia na huduma zinazopatikana huku. Mimi kwa sasa nina miaka 15 hapa King’azi, kwa kweli serikali isonge mbele maana imeonyesha matumaini makubwa kwenye maji hali ya mwanzo na sasa, nampongeza rais kwa jitihada zake anazozifanya kushirikiana na watendaji wake wa chini” alisema ndugu Aidani Mlowe

Pia Kaimu Mhandisi wa maji wa manispaa ya Ubungo Bw Ramadhani Mabula amemuhakikishia mkurugenzi huyo kuendelea kusimamia miradi hiyo kwa umakini zaidi na kuhakikisha inaisha kwa wakati ili wananchi wanufaike na huduma hiyo, nae Mkurugenzi amemuhakikishia mhandisi huyo pamoja na mafundi kuwa ataitembelea miradi hiyo mara kwa mara mpaka pale itakapokamilika.

No comments:

Post a Comment