Waziri wa Kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba akisisitiza jambo wakati akitoa salamu za Wizara yake mbele ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Kassim Majaliwa kwenye sherehe za uzinduzi wa mpango wa matibabu kwa wanachama wa vyama vya ushirika nchini unaojulikana kama Ushirika Afya uliofanyika kijijini Kangeme Kata ya Ulowa, Leo 16 Julai 2018. (Picha Zote Na Mathias Canal-WK)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maeleazo
kutoka kwa Waziri wa Kilimo, Dkt. Charles Tizeba.
(kushoto) wakati alipokagua uuzaji wa tumbaku katika Chama cha
Ushirika cha Msingi cha Kangeme katika Halmashauri ya Ushetu, Julai
16, 2018. Kulia kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Zainab
Telack na wapili kushoto ni Mwenyekiti wa Tume ya Maendeloeo ya Ushirika
Nchini, Dkt. Titus Kamani.
Baadhi ya wakazi wa Halmashauri ya Ushetu Mkoani shinyanga wakimsikiliza kwa makini waziri wa kilimo Mhe. Dkt Charles Tizeba (Mb) wakati akitoa salamu za wizara yake kwenye sherehe za uzinduzi wa mpango wa matibabu kwa wanachama wa vyama vya ushirika nchini unaojulikana kama Ushirika Afya uliofanyika kijijini Kangeme Kata ya Ulowa, Leo 16 Julai 2018.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizindua Fao la
Ushirika Afya ambalo litawawezesha wanaushirika kunufaika na huduma zinazotolewa
na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, kwenye kijiji cha Kangeme katika Halmashauri
ya Ushetu mkoani Shinyanga Julai 16, 2018. Kushoto kwake
ni Waziri wa Kilimo, Dkt. Charles Tizeba, watatu kushoto ni Waziri
wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsi, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu na kushoto ni
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, Bernard Konga.
Waziri wa Kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba akisisitiza jambo wakati akitoa salamu za Wizara yake mbele ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Kassim Majaliwa kwenye sherehe za uzinduzi wa mpango wa matibabu kwa wanachama wa vyama vya ushirika nchini unaojulikana kama Ushirika Afya uliofanyika kijijini Kangeme Kata ya Ulowa, Leo 16 Julai 2018.
Na Mathias Canal-WK,
Ushetu-Shinyanga
Waziri wa Kilimo Mhe Dkt Charles
Tizeba ameagiza timu ya uchunguzi kuzuru katika Halmashauri ya Ushetu Wilayani
Kahama katika Mkoa wa Shinyanga ili kubaini changamoto za uuzaji wa zao la
Tumbaku.
Waziri Tizeba ametoa agizo hilo
Leo 16 Julai 2018 kijijini Kangeme Kata ya Ulowa wakati akitoa salamu za Wizara
ya Kilimo mbele ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Kassim
Majaliwa kwenye sherehe za uzinduzi wa mpango wa matibabu kwa wanachama wa
vyama vya ushirika nchini unaojulikana kama Ushirika Afya.
"Mhe Waziri Mkuu nimewahi kutembea katika masoko mengi ya Tumbaku lakini sikuwahi kufika mahala tukawaona wananchi wananung'unika kama walivyofanya wananchi wa hapa maana yake moja tu kwamba kuna jambo halipo sawa hapa, tumbaku hailimwi Ushetu peke yake inalimwa katika maeneo mengi nchini lakini nilichokiona hapa kinanitia wasiwasi"
"Inaelekea Mhe Waziri Mkuu
katika uteuzi wa Tumbaku kuna kasoro ambapo wakulima wamelima Tumbaku nzuri
lakini inapokuja kuteuliwa inapangiwa madaraja ya chini hivyo inaonekana kama
Tumbaku yao haina Ubora" Alikaririwa Dkt Tizeba
Alisema kuwa timu hiyo ya
uchunguzi itakuwa na jukumu la kufuatilia na kubaini kuwa Uteuzi uliofanyika
ulikuwa wa haki ama vinginevyo na bei ya Tumbaku waliyopewa wananchi sio ya
kutengenezwa bali inatokana na madaraja waliyozalisha.
Dkt Tizeba alikielekeza Chama
cha msingi cha wakulima Mkombozi ambacho bado hakijawalipa wakulima kiasi cha
Dola 21,000 katika kipindi cha miaka minne kuanzia mwaka 2014 mpaka sasa
kuhakikisha msimu huu kiasi hicho cha fedha kinalipwa kwa wananchi kutoka
kwenye makato ya chama chenyewe.
Alisisitiza kuwa atafatilia kwa
karibu jambo hilo ili kuhakikisha kwamba haki ya wananchi inapatikana mwaka huu
kwani mambo kama hayo ndiyo yanayopelekea wananchi kulalamika wakitaka majawabu
kamili.
Alisema, wananchi kuendelea
kulima Tumbaku kwa mikono kunazidi kuwafanya wakulima kuwa tegemezi wa
makampuni kwani kila mwaka wanakopa na kuingizwa katika mkataba ambapo
wakishaingizwa kwenye mkataba huo wafanyabiashara wengine hawawezi kuja
kununua.
Alisema kupitia mikataba hiyo
Tumbaku ya wakulima haiingii katika ushindani kama ilivyo katika Mazao
mengine kama vile korosho na ufuta yanavyoshindaniwa na wanunuzi hivyo
kupelekea bei kupanda na kuongeza kipato kwa wakulima.
"Sasa sisi wakulima
tumejifunga katika mikopo na katika kukopa tunakuwa na mtoa mikopo mmoja ambaye
ni Benki ambazo zinataka kuingia mkataba na makampuni na kuwapa makadirio badae
wanakuja mwenyewe kununua hapo bei itapanda namna gani...? kwa hivyo dawa ni moja
tu wananchi kujifunza kujitegemea kwa kuweka akiba kwa ajili ya uwezalishaji wa
mwaka unaofuata" Alisema Dkt Tizeba
Aliwasihi wananchi hao endapo
wataridhia kuwekwa utaratibu kwa mauzo ya mwaka huu ili msimu wa mwaka 2019
kuwe na utaratibu wa wakulima kujigharamia wenyewe pembejeo bila kuingia kwenye
mikopo ambayo ina riba kubwa ya asilimia 18% mpaka asilimia 20%.
Alisema kuwa mbinu mojawapo ya
kupandisha tija ya bei kwenye zao hilo la Kahawa ni kuongeza wanunuzi kufikia
walau watano kwani kuwa na mnunuzi mmoja tija itaendelea kuwa ndogo huku
wakulima wakiendelea kunyonywa.
Alisema kuwa msimu wa zao la
Pamba utakapofika hakutakuwa na makato wananchi watagaiwa mbegu, dawa na
mabomba ya kupulizia dawa pasina malipo.
Akizungumzia kuhusu Ushika Afya,
Dkt Tizeba aliongeza kuwa Tume ya maendeleo ya Ushirika kwa kushirikiana na
Mfuko wa Taifa wameunda mpango wa matibabu kwa wanachama wa vyama vya Ushirika
nchini ikiwa ni mafanikio yanayoendelea kuonekana katika kuimarisha Ushirika
nchini kwa kuakisi utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi ambayo ndiyo
mkataba kati ya wananchi na serikali katika kipindi cha miaka mitano 2015-2020.
Alisema Ofisi ya Mrajis na Mfuko
wa Bima ya Afya unaendelea na uhamasishaji kwa wanachama wa vyama vya Ushirika
na wakulima ili waweze kujiunga kwenye utaratibu wa matibabu kupitia Ushirika
Afya kwenye mikoa inayolima Korosho, Pamba, Tumbaku, Chai na Kahawa.
Katika hafla hiyo Waziri Mkuu wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Kassim Majaliwa amemkabidhi Waziri wa
Kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba gari moja aina ya Toyota Land Cruiser kwa ajili
ya idara ya kilimo katika Halmashauri ya Ushetu sambamba na pikipiki tatu
zilizonunuliwa kupitia mapato ya ndani kwa ajili ya maafisa ugani ili kuongeza ufanisi
na tija katika ukuzaji wa sekta ya Kilimo katika Wilaya hiyo.
MWISHO.
No comments:
Post a Comment