Thursday, July 12, 2018

DKT ANGELINE MABULA: TUTAENDELEA KUPAMBANA NA CHANGAMOTO ZA ELIMU





Serikali itaendelea kupambana na changamoto zinazoikabili sekta ya Elimu nchini kwa kuhakikisha inaboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia ili kuandaa wataalamu wa kuitumikia nchi na kufikia malengo ya kuwa na uchumi wa viwanda

Kauli hiyo imetolewa na Mbunge wa Jimbo la Ilemela ambae pia ni Naibu Waziri wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe Dkt Angeline Mabula wakati akizungumza na watumishi wa manispaa ya Ilemela, wazee maarufu, viongozi wa dini, viongozi wa serikali za mitaa na watumishi wastaafu wa kata za Nyakato, Nyamhongolo na Buswelu kupitia ziara aliyoianza leo kwa kata zote za jimbo lake yenye lengo la kusikiliza kero, changamoto na kupokea ushauri ili kuliletea maendeleo jimbo hilo ambapo amewaasa walimu kuhakikisha wanatekeleza wajibu wao wakati Serikali ikiendelea kutatua changamoto zinazowakabili ikiwemo kupandishwa madaraja, kulipa madeni na kuboresha mazingira ya kufundishia

‘… Serikali itaendelea kutatua changamoto za Elimu, Lakini hili lisitukatishe tama kutimiza wajibu wetu tukifanya bora liende hasara itakuwa kwetu kwani hata kama huyu mwanafunzi hata kuwa ofisini lakini ndo atakuwa kiongozi wako wa mtaa, ndo atakuwa mshauri wako kwenye mambo fulani, lakini wewe hukumpa elimu anayostahili na ukistaafu tunategemea huyo huyo akuhudumie…’ Alisema mia

Aidha Mhe Mabula amewaasa watumishi wote wa Umma kufanya kazi kwa bidii na weredi ili kulisaidia taifa huku akiwataka wastaafu kutoa mchango wao kwa jamii kupitia uzoefu walionao ili kujiletea maendeleo

Kwa upande wake kaimu mkurugenzi wa manispaa ya Ilemela ndugu Daniel Batare aliyeambata na wataalamu wa manispaa hiyo mbali na kujibu hoja zilizoibuka kupitia ziara hiyo ametaja miradi mbalimbali inayotekelezwa ndani ya manispaa yake ikiwemo ujenzi wa barabara kumi na tano ambazo wakandarasi wamekwisha tia saini kuanza ujenzi wake.

Akihitimisha ziara hiyo kwa niaba ya madiwani wa kata za Nyamhongolo, Buswelu na Nyakato, Diwani wa kata ya Nyakato Mhe Alfred Wambura amemshukuru mbunge huyo kwa ziara aliyoifanya huku akimuomba kuendelea kuzitafutia ufumbuzi changamoto zilizoibuliwa kupitia ziara hiyo ikiwemo migogoro ya ardhi, changamoto za kiutumishi na kuendelea kutekeleza miradi ya maendeleo kwa pamoja.

Wakati huo huo akiwa makao makuu ya manispaa Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula amepokea ugeni kutoka shule ya Derby Grammar ya nchini Marekani ikiwa ni shule rafiki wa shule ya msingi Ibeshi iliyopo Nyakato ambayo mpaka sasa imesaidia ujenzi wa madarasa, umeme, maji, ujenzi wa uwanja wa mpira na vifaa vya kujifunzia na kufundishia.

' Ilemela ni yetu, tushirikiane kuijenga'
Imetolewa na
Ofisi ya mbunge
Jimbo la Ilemela
10.07.2018

No comments:

Post a Comment