Friday, June 15, 2018

Mkuu wa Majeshi Awataka Vijana Kujiunga JKT Kupata Stadi za Kazi ziwasaidie Kujiajiri

Posted On: June 7th, 2018
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi  Jenerali Venance Mabeyo amewahamasisha vijana kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa ili waweze kupata stadi za ufundi na hatimaye wajiajiri badala ya kutegemea kuajiriwa na Serikali.
Jenerali Mabeyo ametoa ushauri huo wakati alipokutana na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu na Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Simiyu mjini Bariadi Juni 07, 2018.
Mabeyo amesema vyombo vya habari vinapaswa kuwahamasisha vijana kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa ili waweze kupata stadi za ufundi na hatimaye wajiajiri na hivyo waondokane na dhana ya kuajiriwa  .
“Vijana tunaowachukua JKT ni kwa ajili ya kuwapa elimu na stadi za kazi ili hata kijana akikosa nafasi katika vyombo vya Ulinzi na Usalama anaweza kurudi kijijini akafanya vitu vya maendeleo, mimi nadhani watu wanahamsishana vibaya kuwa kila anayekwenda JKT lazima aajiriwe,  ipo haja ya kubadili mtazamo” alisema Jenerali Mabeyo
“Jeshi linachukua vijana elfu ishirini kwa mafunzo, wanaochukuliwa na vyombo vya ulinzi na usalama hawazidi vijana 2000 sasa hawa wengine 18,000 wanaenda wapi, kama mawazo yatakuwa ni kwenda JKT ili kuajiriwa hatutafanikiwa lakini kama watakwenda JKT kujifunza stadi za kazi kuwasaidia ili ziwasaidie kujiajiri na kubadili maisha yao tutafanikiwa sana” alisisitiza
Katika hatua nyingine Jenerali Mabeyo ametoa pongezi kwa  juhudi zinazofanywa na Mkoa wa Simiyu katika mkakati wa Kilimo cha Umwagiliaji ili kuwa na ziada ya chakula cha kutosha.
“Suala la umwagiliaji halikuwepo katika fikra za watu wengi, walio wengi wanategemea mvua na isiponyesha hawalimi na  maisha yanakuwa duni  wanaanza kuilalamikia Serikali, lakini sisi hapa tunayo maji ya Ziwa Victoria, Mkuu wa Mkoa nawapongeza sana kwa juhudi zinazofanywa katika kilimo cha Umwagiliaji, zitasaidia kuwatoa wananchi kwenye ufukara” amesema  Mabeyo.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Anthony Mtaka amesema mkoa huo umeweka malengo ya kujitosheleza kwa chakula na kupitia mkakati wa kuwa na mradi wa kilimo cha umwagiliaji katika bonde la Mwamanyili wilayani Busega, ambapo amebainisha kuwa Benki ya Maendeleo ya Kilimo imeahidi kutoa shilingi bilioni 12kwa ajili ya mradi huo.
“ Lengo letu kama mkoa ni kuifanya wilaya ya Busega kuwa eneo ambalo linafanya vizuri katika kilimo cha umwagiliaji kwa kuwa lina maji ya uhakika ya Ziwa Victoria, Benki ya Kilimo wameahidi kutupa shilingi bilioni 12 kwa ajili ya mradi wa Kilimo cha Umwagiliaji wa Mwamanyil” alisema Mtaka.
Akizungumzia suala la elimu Mtaka amesema mkoa huo umejipanga kiushindani ambapo madarasa ya mitihani. yatakuwa na makambi ya kitaaluma  ambazo zitawakutanisha wanafunzi kwa ajili ya kupitia maeneo yaliyo magumu ili waweze kujiandaa vema na mitihani ya Kitaifa.
MWISHO

No comments:

Post a Comment