Friday, June 15, 2018

Mkurugenzi TAA awasamehe wote waliomkwaza





Na Mwandishi Wetu

KAIMU Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA),Bw.  Richard Mayongela amesema amewasamehe wale wote waliomkwaza na kumuudhi katika utekelezaji wa majukumu yake kwa bahati mbaya au kwa makusudi aliteleza kama binadamu.

Kauli hiyo aliitoa juzi wakati wa kufuturu katika futari aliyoiandaa na kufanyika eneo la karibu na Jengo la Kwanza la abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA-TB1), ambapo ilihusisha wafanyakazi wa TAA na wadau wengine wanaofanyakazi mbalimbali na Mamlaka hiyo.

“Naomba tusameheane pale tulipokoseana, sisi ni binadamu hatuko kamili katika namna moja au nyingine tumekwazana katika kutekeleza majukumu yetu, kwa bahati mbaya mimi nikiwa ofisini nakuwa ni Mwajiri na halafu wenzangu upande wa pili wanakuwa waajiriwa, hivyo katika kutekeleza majukumu yetu naweza kuteleza mimi ni binadamu naombeni katika mwezi huu Mtukufu wa Ramadhan tusameheane, name nimewasamehe wote,” amesema Bw. Mayongela.

Hata hivyo, Bw. Mayongela amesema dini zetu siziwe vigezo vya kubaguana, kwa kuwa tunashiriki katika shughuli mbalimbali na kufanya kazi pamoja, ambapo TAA wapo wafanyakazi Waislam na Wakristo, hali kadhalika kwa wadau wa Mamlaka wapo wa madhehebu hayo, na wanafanyakazi pamoja.

Pia Bw. Mayongela amesema ni imani yake wataendeleza yale mema waliyokuwa wakiyafanya kwa kipindi chote cha mwezi Mtukufu wa Ramadhan, yakiwemo ya kudumu katika sala na kujinyima na kumlilia Mwenyezi Mungu aweze kutusaidia kwa kila jambo na ndio mtakayoyaendeleza hata baada ya Ramadhan.

Hata hivyo, Bw. Mayongela amesema tukio hili la Iftah liwe ni ishara na mwanzo wa ushirikiano mzuri baina ya TAA na wadau wake wanaojishughulisha na shughuli mbalimbali kwenye Kiwanja cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), ambapo hata vitabu vya dini vinazungumzia ushirikiano, ambapo ametaka asiwepo mtumwa wala mtwana na asiwepo bwanyeye wala bosi, kwa kuwa sisi wote tupo sawa mbele ya Mwenyezi Mungu na tunahaki sawa.  

“Nawapenda sana ndugu zangu Waislam na ningefurahi zaidi kote kungekuwa na mikeka na tukaa chini hiyo ni ishara wote tupo sawa kwa Mwenyezi Mungu na hakuna wa juu, katikati na chini, kwa sababu kuna maisha baada ya maisha ya hapa Duniani,” amesema Bw. Mayongela.

Pia Bw. Mayongela ametoa shukrani alizopewa na Serikali kwa wadau wote kwa kufanikisha huduma bora kwa ndege kubwa ya Emirates Airbus 380 iliyokuwa ikielekea Mauritius na kutua kwa dharura tarehe 24 April, 2018 kutokana na hali mbaya ya hewa nchini huko, ambapo tukio hilo ni la kihistoria na lilizungumzwa katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambapo pia  amefungua milango wazi kwa wadau kufika ofisini kwake kwa lengo la kujenga na kuendeleza viwanja vya ndege Tanzania. 

Naye Katibu Mtendaji wa Chama cha Watoa Huduma za Ndege (TAOA), Bw. Laurence Paul amempongeza Kaimu Mkurugenzi wa TAA, Bw. Mayongela kwa kuwa wa kwanza kuandaa Iftah hii tangu kuanzishwa kwa Mamlaka hii mwaka 1999, ambapo imeonesha ni namna gani anaushirikiano na upendo mkubwa kwa wadau wake wote.

“Nimefanyakazi hapa kwa muda mrefu tangu mwaka 1971 ingawa nilikuwa nikihamishwa na kurudishwa tena hapa TB1, lakini sikuwahi kuona kiongozi aliyetukutanisha kwa jinsi hii, Mkurugenzi mkuu umetuweka karibu na unatambua kuwa ukaribu wa wadau wako ndio wepesi wa kazi yako, kwani tukiwa hatuko karibu itakuwa shida kwako kutuongoza, hivyo napenda kukupongeza kwa kuwa na mawazo haya ya kutuleta pamoja,” amesema Bw. Paul.

Bw. Paul amesema hatua hii ya Iftah pamoja itasaidia kuweka wadau pamoja na kuweka usalama Kiwanja kwani kinauzika kutokana na kuwa na usalama.

Kwa upande wa Imam wa Msikiti ulipo karibu na Jengo la Kwanza la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA-TB1), Shehe Mahmoud Rajab naye amemshukuru Mkurugenzi Mkuu na kumuombea dua ili aendelee na adhima yake ya kuwaleta wadau pamoja, ambapo haijawahi kutokea.

“Tunashukuru kwa uhusiano huu wa Mkurugenzi huyu mpya kwani haijawahi kutokea kuunganisha watu namna hii, na tunashukuru na sisi Waislam tunasehemu ya kuabudia tukiwa maeneo ya kazi kwani kule Njiapanda ni mbali sana, tunashukuru sana ten asana,” amesema Imam huyo.

MWISHO.

No comments:

Post a Comment