Watumishi wa huduma za afya wametakiwa
kujaza taarifa sahihi za walengwa wanaonufaika na mpango wa kunusuru kaya
masikini TASAF ili kuepuka tafsiri tofauti za taarifa zinazotolewa na vituo vya
afya.
Kauli hiyo imetolewa leo na mkurugenzi
wa manispaa ya Ilemela ndugu John Wanga wakati akifungua kikao kazi cha
siku moja kwa watoa huduma za afya kutoka vituo vyote vya afya vinavyohudumia
walengwa hao ndani ya manispaa yake ambapo amewaasa kuhakikisha wanajaza
taarifa sahihi za walengwa hao pindi wanapofata huduma katika vituo vyao
sambamba na kuelekeza juu ya kuwepo watumishi maalumu watakaohusika na upitiaji
wa fomu za walengwa hao ili kuongeza ufanisi na uwajibikaji katika utoaji wa
huduma.
‘… Wanapokuja walengwa wa
mpango wa kunusuru kaya masikini kufata huduma katika vituo vyenu vya afya
nawaomba sana mjaze taarifa sahihi sio mnajijazia tu bora liende pia
mtambue mnapojaza taarifa zisizo sahihi zinapokwenda kutafsiriwa lazima
zitaleta picha tofauti …’ Alisema
Aidha mkurugenzi huyo ameongeza
kuwa hata vumilia mtumishi yeyote atakaekwenda kinyume na maelekezo hayo na
hatua kali za kinidhamu zitachukuliwa kwa mtumishi yeyote ataebainika kutoa
taarifa zisizosahihi na asijefuata utaratibu.
Kwa upande wake mratibu wa
TASAF manispaa ya Ilemela ndugu Frank Ngitaoh mbali na kubainisha mafanikio
yaliyopatikana kupitia mpango huo ikiwemo kukwamua walengwa zaidi ya 2509
katika umasikini kwa kuwapa mtaji ili kuanzisha miradi midogo midogo ya
kukuza kipato amebainisha juu ya mkakati endelevu walionao utakaosaidia
walengwa hao kujikwamua kiuchumi hata baada ya kuisha kwa mpango huo kwa
kuwaunganisha walengwa kupitia vikundi ili kushiriki shughuli za kujiongezea
kipato.
Nae mwakilishi wa mganga mkuu
wa wilaya hiyo ambae pia ni mratibu wa mpango wa huduma za afya ya jamii
iliyoboreshwa (CHF) Bi Gisela Orasa mbali na kushukuru kwa kufanyika
kikao kazi hicho amewataka wahudumu wa afya na wawezeshaji wa mpango wa
kunusuru kaya masikini kushirikiana kwa pamoja katika kuwaelimisha walengwa wa
mpango huo kujiunga katika mfuko huo wa huduma za afya ili waweze
kujihakikishia upatikanaji wa huduma bora za afya huku akitoa rai kwa wahudumu
wenzake juu ya kuzingatia weredi na taaluma yao katika kutekeleza majukumu yao
ya kila siku.
Akihitimisha kikao kazi hicho afisa
ufuatiliaji wa mpango huo ndugu Kagwe Samson amewataka wahudumu hao wa afya
kuwa wakarimu pindi wanapowahudumia walengwa wa mpango wa kunusuru kaya
masikini ili kuondoa unyanyapaa sanjari na kwenda sambamba na malengo ya
serikali chini ya mheshimiwa Rais Daktari John Magufuli ya kupambana na
umasikini unaolikabili kundi kubwa la watu katika jamii.
No comments:
Post a Comment