Wednesday, June 13, 2018

KATIBU MKUU CCM DKT KAKURWA ATANGAZA KUHAMIA DODOMA

Leo 13 Juni 2018 Mamia ya wananchi na wanachama wa CCM wamemlaki Ndg. Bashiru Ally Kakurwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) alipowasili kwa mara ya kwanza jijini humo kama Katibu Mkuu wa CCM na ikiwa ni kituo chake kikuu cha kazi.

Mamia ya wananchi na wana CCM walikusanyika katika uwanja wa ndege wa Dodoma na katika Ofisi za Makao Makuu ya CCM (White House).

Akizungumza na wananchi wa jiji la Dodoma waliofika kumlaki, wanachama wa CCM, viongozi wa CCM kutoka Mkoa wa Dodoma na watumishi wa Chama Cha Mapinduzi, Ndg. Bashiru amesema amepewa dhamana kubwa na wana CCM, dhamana ya kusimamia Mageuzi Makubwa ambayo yanakirejesha Chama chetu kwa wanachama na katika misingi ambayo kwayo Chama Cha Mapinduzi kiliasisiwa.

Ndg. Bashiru amegusia kwa ufupi kazi kubwa iliyo mbele ya wana CCM kwa ujumla kuwa ni kuhakikisha kazi nzuri ya kuendelea kuhuisha uhai wa Chama Cha Mapinduzi katika ngazi ya Mashina, Matawi na Kata inaimarishwa maradufu, na kwamba uhai wa Chama uende sambamba na vikao vya Chama kukaa ili kuimarisha usimamizi wa rasilimali zetu za Chama kote nchini.

Aidha Ndg. Bashiru amezuangumzia hali ya maslahi ya watumishi wa Chama Cha Mapinduzi bado si ya kuridhisha, na akatumia fursa hiyo kuwapongeza watumishi wa CCM kwa moyo wao wa kujitolea, utii na nidhamu ya hali ya juu licha ya changamoto walizonazo.

"Nitafanya kazi kwa bidhii kuimarisha misingi ya Chama kujitegemea na tutaboresha maslahi ya watumishi, hiki ni kipaumbele namba moja na ndio Maelekezo na msimamo wa Ndg. John Pombe Joseph Magufuli, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)" amesema Ndg. Bashiru Ally Katibu Mkuu wa CCM.

Akizungumzia kuhusu Mageuzi yanayofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Ndg. John Pombe John Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amesema kubana mirija ya dhuluma na unyonyaji iliyowekwa na wasioitakia mema nchi yetu kutoka nje ya nchi na vibaraka wao hapa nchini, hakutawafurahisha wanufaika wa mfumo wa dhuluma na unyonyaji ndani na nje ya nchi. Ni kazi yetu kama Chama kumlinda na kutetea Ndg. Magufuli Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Tanzania.

"Kuna umuhimu wa kuimarisha Chama Cha Mapinduzi, kwasababu mambo haya ya mageuzi yanahitaji chombo cha uongozi, huwezi ukajenga uchumi wa kitaifa bila chombo cha uongozi, huwezi ukapambana na ufisadi, ukaimarisha uwajibikaji na uwazi, ukatoa huduma za kijamii kwa wanyonge bila ya kuwa na chombo imara na chombo imara kinachotegemewa na watanzania ni Chama Cha Mapinduzi na katika Ilani yetu ya Uchaguzi kuna sura mahususi inayohusu uimarishaji wa Chama chetu"  Alisema Ndg. Bashiru Ally Kakurwa Katibu Mkuu wa CCM.

Akitoa salamu za shukrani Mzee Job Lusinde, Mwenyekiti wa Baraza la Wazee la Mkoa wa Dodoma amesema ameguswa sana na kauli ya Katibu Mkuu kwamba tunakirejesha Chama chetu katika misingi ya TANU na ASP. Mzee Lusinde amemtakia kwa niaba ya wazee wa Jiji la Dodoma Afya njema, busara, mafanikio makubwa, mfungo mwema wa Mwezi wa Ramadhani na Sikukuu njema ya Eid.

Shughuli ya mapokezi imehudhuriwa na wananchi, wanachama wa CCM, viongozi wa CCM wa ngazi zote Mkoa wa Dodoma wakiongozwa na Ndg. Godwin Azaria Mkanwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma pamoja na Mzee Pancras Ndejembi na Mzee Job Lusinde

Imetolewa na,

IDARA YA ITIKADI NA UENEZI
CHAMA CHA MAPINDUZI (CCM)
OFISI YA MAKAO MAKUU - DODOMA

No comments:

Post a Comment