Sunday, June 17, 2018

DKT TIZEBA AUNGANA NA MAMIA YA WAOMBOLEZAJI MAZISHI YA MZEE JULIUS MABULA

Na Mathias Canal, WK-Mwanza

Jana 16 Juni 2018 Waziri wa Kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba pamoja na Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Mary Mwanjelwa waliungana na mamia ya waombolezaji Jijini Mwanza kwenye mazishi ya Mzee Julius Makono Mabula aliyezikwa katika makaburi ya Romani Catholic Mtaa na Kata ya Kirumba.

Mzee Mabula alikuwa mume wa Mbunge wa Jimbo la Ilemela Jijini Mwanza ambaye pia ni Naibu Waziri wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe Dkt Angeline S.L Mabula. 

Viongozi mbalimbali wa serikali na chama cha Mapinduzi kuanzia ngazi ya shina mpaka Taifa na vyama vingine vya upinzani wameshiriki katika hatua zote za safari ya mwisho ya Mzee huyo ambaye enzi za uhai wake alikuwa na ushawishi mkubwa katika jamii na hata katika Kanisa la Roman Katoliki Mwanza.

Kifo cha Mzee Mabula kilitokea siku ya Jumatano Juni 13, 2018 katika hospitali ya Bugando Jijini Mwanza alipokuwa akipatiwa matibabu.

Kwa niaba ya watumishi wa Wizara yake Dkt Tizeba amesema kuwa kifo cha  mume wa Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kimeacha pengo na huzuni kubwa kwa familia, kanisa na jamii kwa ujumla lakini watanzania wanapaswa kuwaombea marehemu wote ili wapumzike kwa amani.

Akitoa salamu za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt. John Pombe Magufuli, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe William Lukuvi alisema kuwa Rais amepokea kwa masikitiko makubwa kifo hicho kwani Mzee Mabula amekuwa mume bora na mfano katika jamii.

Rais Magufuli ametoa pole kwa mama mjane Dkt Angelina Mabula na wana Chama wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Ilemela kwa kuondokewa na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya Mstahafu na Mwenyekiti wa Jumuya ya Wazazi Kata ya Kirumba Mstahafu.

Marehemu aliwahi kuwa katibu wa Timu ya soka ya Pamba ya Mwanza na kuifanya Timu hiyo kuwika na kutamba ndani ya Tanzania na Nje ya Nchi.

Bwana ametoa na Bwana Ametwaa jina lake lihimidiwe. Ameni 

MWISHO.

No comments:

Post a Comment