Na Grace
Gwamagobe-Songwe
Waziri wa Maji na
Umwagiliaji Mhandisi Isaack Kamwelwe ametahadharisha kuwafukuza kazi na
kuwashitaki wahandisi wa serikali wanaokosa uzalendo na kuhujumu miradi ya maji
katika hatua ya usanifu na usimamizi kwa kupitisha vifaa vilivyo chini ya
viwango.
Mhandisi Kamwelwe
ametoa tahadhari hiyo wakati wa ziara yake Mkoani Songwe ya kukagua utekelezaji
wa miradi mitatu ya maji ya Iyula na Itaka katika halmashauri ya Mbozi, mradi
wa Umwagiliaji Naming’ongo katika halmashauri ya Momba na mradi wa Maji Tunduma
katika halmasahuri ya Tunduma.
“Miradi mingi
inakamilika na kuzinduliwa na viongozi wakubwa wa kitaifa lakini mabomba
yanaanza kupasuka muda mfupi tu baada ya wananchi kuanza kupata maji kwakuwa
hayana viwango, wahandisi badilikeni na hili likitokea hauna ajira na
kushitakiwa juu”, amesisitiza Kamwelwe.
Ameongeza kuwa
kukamilika kwa miradi ya maji hakutakuwa na tija endapo shughuli za utafiti wa
vyanzo vingine imara vya maji hazitafanyika pamoja na kutunza vyanzo vya maji
vilivyopo kwa ajili ya uendelevu wa miradi hiyo kwa muda mrefu.
“Hatutaki kusikia
mradi unatoa maji kwa muda mfupi kisha maji yanaisha kwenye vyanzo, hivyo
naagiza taasisi ya bonde la ziwa Rukwa washirikiane na taasisi nyingine pamoja
na ofisi za wakuu wa wilaya kutafuta vyanzo vingine vya maji pamoja na ulinzi
wa vyanzo vilivyopo”, amebainisha Mhandisi Kamwelwe.
Kwa Upande wao
wananchi wameiomba serikali kuwepo kwa uwazi na ushirikishwaji katika hatua
zote za ujenzi wa miradi tangu hatua ya usanifu ili kujenga uelewa juu ya
miradi hiyo na kuondoa migogoro.
Ujenzi wa miradi ya
maji ya Iyula, Itaka na Tunduma inatarajiwa kutoa huduma ya maji kwa wananchi
takribani laki moja ambao watakuwa wanapata maji kwa umbali usiozidi mita 400
sawa na mwongozo wa sera ya maji ya mwaka 2002.
No comments:
Post a Comment