Na Stella Kalinga, Simiyu
Baraza la Uongozi wa Chuo cha Mipango
Dodoma limeushukuru , uongozi wa Mkoa wa Simiyu kwa kukubali kutoa
eneo la ekari 50 bure kwa ajili ya ujenzi wa Tawi jipya la chuo hicho , katika
Kata ya Nyakabindi Halmashauri ya Mji wa Bariadi.
Shukrani hizo zimetolewa na Kaimu Mwenyekiti wa Baraza la
Uongozi wa Chuo cha Mipango Bibi.Mugabe Mtani , katika mazungumzo maalum na
viongozi wa Mkoa wa Simiyu muda mfupi kabla ya kikao cha Baraza hilo
kilichofanyika mkoani Simiyu.
Kaimu Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo cha Mipango
Bibi. Mugabe Mtani ameshukuru kwa niaba ya Chuo
hicho kwa kupewa eneo hilo ambalo litawawezesha kujenga miundombinu
ya kutosha ya chuo hicho katika Mkoa wa Simiyu.
“Tunashukuru sana uongozi wa Mkoa wa Simiyu kwa kutupa
hili eneo kubwa katika wakati huu ambao sisi tunaona ni wakati muafaka kwa
sababu tulikuwa kwenye mkakati wa kutafuta eneo la kujenga, pale Mwanza tuna
eneo ambalo kama tungelitumia lingetugharimu fedha nyingi kuliko hili la Simiyu
kwa sababu liko kwenye mawe” alisema Mtani.
Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Chuo cha Mipango, Hozen Mayaya
amesema iwapo chuo hicho kitakamilika kujengwa kitasaidia kutoa mafunzo
ya maendeleo vijijini na hivyo kusaidia upatikanaji wa watalaam hapa nchini
wakiwemo wa mipango pamoja na kusaidia katika ufanyaji wa tafiti mbalimbali.
Ameongeza kuwa upatikanaji wa eneo hilo utasaidia lengo la Chuo
la kuwa vituo vingi kadri mahitaji yanavyoongezeka jambo ambalo litasaidia pia
kusogeza huduma karibu na wananchi.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi ambako eneo hilo
lipo, Bw. Melkizedeck Humbe amesema Chuo cha Mipango kitapojengwa Mkoani Simiyu
kitakuwa msaada mkubwa kwa Mkoa huo ambao unajipambanua kwa Uchumi wa viwanda.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amesema kuwepo
kwa chuo hicho kutaongeza hamasa ya elimu kwa vijana wanaomaliza elimu ya
sekondari na kidato cha sita kujiunga na vyuo vya elimu ya juu ,huku akitoa
wito kwa Taasisi zingine za umma na binafsi kuwekeza katika sekta ya
elimu.
“ Sisi kama Mkoa tunatoa fursa kwa Wakuu wote wa Vyuo Vikuu hapa
nchini wanaotaka kujenga matawi ya Vyuo vyao ili waondokane na kulipa fedha
nyingi kwa ajili ya pango la majengo, mkoa wa Simiyu unawaakaribisha na
tunawahakikishia upatikanaji wa Ardhi Bure” alisema Mtaka.
MWISHO:
No comments:
Post a Comment