Saturday, May 26, 2018

Bunge lapitisha Bajeti ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka 2018/19



Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 25 Mei, 2018, lilipitisha  Makadirio ya Jumla ya Shilingi 1,692,286,014,000 kwa ajili ya matumizi ya Wizara ya Nishati na Taasisi zake kwa Mwaka wa Fedha 2018/19.

Baada ya kupitishwa kwa Bajeti hiyo, katika kikao na Watendaji wa Wizara na Taasisi, Waziri wa Nishati  Dkt. Medard Kalemani alitoa pongezi za pekee kwa Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu kwa namna ambavyo amekuwa akisimamia  utekelezaji wa majukumu ya Sekta na kueleza kuwa ndani ya kipindi kifupi alichokaa wizarani tangu kuteuliwa kwake, Naibu Waziri amefanya kazi kubwa.

Pia, alipongeza  Watendaji   na Watumishi wa Wizara na Taasisi  zake kwa ushirikiano mkubwa waliouonesha wakati wote wa utekelezaji wa Majukumu ya Wizara.

Alieleza kuwa, pongezi zilizotolewa kwa Wizara  na Wabunge wakati wa kuwasilisha Bajeti ni pongezi za Wizara nzima na hivyo kuwataka watumishi wote wa wizara  kuzilinda pongezi hizo, kujipima na kujitafakari na kutekeleza yote yaliyoshauriwa na Wabunge hao.

Aliwataka watumishi wote wa wizara ya Nishati kuwasilikiza wananchi kwa kuwa kufanya hivyo kunatoa nafasi ya kuchuja mambo na kuyafanyia kazi kikamilifu.

Pia, aliwataka watumishi wote wa Wizara na Taasisi kulala na masuala ya muhimu vichwani mwao kwa ajili ya kuendeleza sekta.

Kwa upande wake, Naibu Waziri Subira Mgalu alipongeza ushirikiano uliooneshwa na watumishi wa Wizara na Nishati na taasisi zake na hivyo kuwataka kujipanga kwa ajili ya utekelezaji wa  majukumu ya Bajeti ya Mwaka wa  Fedha 2018/19.

Naye, Katibu Mkuu Mkuu wa Wizara ya Nishati  na Dkt. Hamisi Mwinyimvua, alisifu ushirikiano uliopo katika Wizara na Taasisi zake na hivyo kuwataka watumishi wote kuendelea na ari hiyo.

No comments:

Post a Comment