Na Stella Kalinga, Simiyu
Balozi wa Indonesia hapa nchini Prof.Dkt. Ratlan Pardede
amewaahidi viongozi wa Mkoa wa Simiyu kuwa atawaalika wawekezaji wa Viwanda vya
nguo, viwanda vya kuchakata ngozi na viwanda vya
kutengeneza mbolea kutoka nchini Indonesia kuja kuwekeza Mkoani Simiyu.
Mhe. Balozi Pardede ameyasema hayo Mei 15, alipokuwa katika
ziara yake Mkoani Simiyu mara baada ya kutembelea kiwanda cha Kuchambua pamba
cha Kasoli Alliance kilichopo Wilayani Bariadi na Kiwanda cha kuchakata ngozi
cha Senani wilayani Maswa.
Amesema atawaalika
wafanyabiashara kutoka nchini Indonesia kuja Simiyu ili wakutane na viongozi wa
mkoa huo pamoja na wafanyabiashara wenzao kujadili juu ya kuongeza uzalishaji
wa pamba bora, bei ya pamba na kuona namna ya kuuza pamba ya Simiyu (Tanzania)
nchini Indonesia moja kwa moja.
Pamoja na kuahidi
kuwaalika wawekezaji wa viwanda vya kuchakata bidhaa za ngozi, Balozi Pardede
akiwa katika kiwanda cha kutengeneza bidhaa za ngozi cha Senani Maswa ameahidi
kusaidia kuleta wataalam kutoka Indonesia watakaosaidia wafanyakazi wa kiwanda
kutengeneza bidhaa bora za ngozi na kuwapeleka wafanyakazi hao Indonesia
kujifunza na kupata maarifa na uzoefu.
Meneja mkuu wa Kiwanda
cha kuchambua pamba cha Alliance Bw. Boaz Ogola amesema ujio wa Balozi wa
Indonesia ni fursa kubwa kwa wanunuzi wa pamba kutokana na nchi hiyo kuwa na
uhitaji mkubwa wa pamba kwa ajili ya viwanda vya nguo na utafungua milango ya
majadiliano na wafanyanyabiashara wa Indonesia na kufanya biashara ya moja kwa
moja.
Naye Mkuu wa Mkoa wa
Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amesema wamezungumza na Mhe.Balozi kumuomba awaalike
wafanyabiashara wa Indonesia Mkoani humo kuwekeza kwenye viwanda vya kuchakata
ngozi, ili viwanda vidogo vilivyopo na vitakapojengwa viwanda vikubwa uwekezaji
wake uanze na malighafi kutoka ndani ya mkoa.
Aidha, Mtaka amesema
Simiyu kama mkoa unaojihusisha na kilimo na unaopakana na mikoa inayofanya
shughuli za kilimo unaona ipo haja ya kuwa na wawekezaji wanaotengeneza mbolea
jambo ambalo limepokelewa na Mhe. Balozi na kuahidi kulifanyika kazi kwa
kuwaalika wawekezaji.
“Tumezungumza na Mhe.
Balozi na ameona uhitaji na umuhimu wa kuwakaribisha wawekezaji kulingana na
mkoa jinsi ulivyo, jambo hili la kupata wawekezaji kwenye uzalishaji wa mbolea
lipo pia katika mwongozo wetu wa uwekezaji kwa ajili ya kusaidia mikoa
inayotuzunguka kama sehemu ya kuboresha eneo la kilimo” alisema.
Wakati huo huo Mtaka
amesema wamezungumza na Mhe. Balozi kuona uwezekano wa Mkoa wa Simiyu kuwa
mwenyeji kufanya mkutano wa Wizara ya Kilimo ya Indonesia na Wizara ya kilimo
ya Tanzania mkoani Simiyu ambao unatarajia kufanyika mwezi Septemba mwaka huu.
Mhe.Balozi alipata
nafasiya kutembelea kiwanda cha Chaki wilayani Maswa, ambapo Mkuu wa Mkoa
amesema Serikali imetoa shilingi bilioni 8.2 kwa ajili ya upanuzi wa kiwanda
hicho na ujenzi wa kiwanda cha vifungashio, hivyo akawataka vijana wanaofanya
kazi katika kiwanda hicho kufanya kazi kwa bidii ambapo amewahakikishia kuwa
baada ya upanuzi wa kiwanda hicho watakuwa waajiriwa wa kudumu.
Mhe. Balozi bado
anaendelea na ziara yake mkoani Simiyu ambapo amepata nafasi ya kutembelea
kiwanda cha kuchambua pamba Kasoli Alliance, Kiwanda cha kutengeneza bidhaa za
ngozi na kiwanda cha chaki wilayani Maswa.
MWISHO.
No comments:
Post a Comment