Na Mathias Canal, Mwanza
Waziri Wa mambo ya ndani Mhe. Dkt Mwigulu Lameck Nchemba amewasihi viongozi mbalimbali wa dini nchini wakiwemo maaskofu na Mashekh kutumia muda wao mwingi kwa kutembelea mikoa mbalimbali nchini kunapotokea zaidi matukio ya kikatili ikiwemo mauaji ili kuhubiri injili wananchi wawe na hofu na Mungu jambo litakalopelekea kupunguza ukatili na watu kumjua Mungu.
Dkt Nchemba ameyasema hayo Wakati akimuwakilisha Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Mama Samia Suluhu alipokuwa akihutubia mamia ya waamini kwenye Tamasha La muziki Wa Injili lililoandaliwa na Ndg Alex Msama Mkurugenzi Mtendaji Wa Kampuni ya Msama Promotion ambaye huratibu matamasha hayo kila mwaka.
Dkt Mwigulu aliwasihi wananchi kwa mshikamano na wingi wao Kuendelea kumuombea Rais Wa Jamhuri ya Muungano Wa Tanzania Mhe. Dkt John Pombe Magufuli kwani anafanya kazi kubwa katika kuwatumikia watanzania ikiwa ni pamoja na usimamizi mzuri Wa Rasilimali za Taifa ambazo amekusudia kuwanufaisha watanzania wote kupitia uchumi fungamanishi.
Alisema nia na Dira ya Rais Magufuli ni msisitizo mkubwa Wa umuhimu Wa maslahi kwa watanzania huku akiwasihi maaskofu Wa makanisa yote nchini kuendelea kueneza neno la Mungu kwani matukio yanayotokea ya mauaji yanasababishwa na wananchi kutomjua Mungu kwa kufanya imani za kishirikiana na ukatili kwa watoto, ubakaji wa wanawake, ulawiti, unyanyasaji wa wazee na wananchi wengi kwa ujumla wake.
Katika tamasha hilo Dkt Mwigulu pia Amezindua albamu ya Msanii nguli Wa nyimbo za injili nchini Tanzania Bi Rose Muhando ijulikanayo kama USIVUNJIKE MOYO na kununua albamu hiyo kwa Shilingi 500,000 huku tamasha hilo likichagizwa na waimbaji 17 Wa ndani na nje ya nchi.
Akijibu risala ya Kampuni ya Msama Promotion kuhusu wizi Wa kazi za wasanii, Mhe Mwigulu alisema kuwa serikali inatambua kadhia hiyo inayowakumba wasanii Wa dini nchini hivyo atawasiliana na Wizara ya Habari, sanaa, utamaduni na Michezo ili kuweka msisitizo katika kuratibu shughuli ya kuepusha wizi Wa wasanii.
Awali akisoma risala ya kampuni ya Msama Promotion Askofu Zenobiasi Sisaya Wa kanisa la Filadephia, alisema kuwa Watanzania kwa umoja wao wanapaswa kudumisha amani na mshikamano ambapo pia amesisitiza serikali kupigia chepuo kwa kuzitambua kazi za wasanii na kuwatia nguvuni wale wote wanaochakachua kazi za wasanii.
Alisema kuwa hali hiyo inawafanya wasanii wanaotumia kazi kubwa kiakili na kimwili kutengeneza kazi hizo lakini pasina kuwa na faida kwao kwani wezi hao wanazalisha kazi nyingi ambazo zipo chini ya kiwango na hatimaye kulikosesha faida Taifa kwa kutolipa kodi.
Aliiomba serikali kupitia Wizara ya mambo ya ndani ya nchi na Wizara ya Habari, sanaa, utamaduni na Michezo kuwachukulia hatua za haraka wezi Wa kazi hizo za wasanii kupitia wakuu Wa wilaya na mikoa kufanya msako endelevu kwa wote wanaofanya jukumu hilo.
Dhifa hiyo ya Tamasha la Pasaka imehudhuriwa pia na Mkuu Wa Mkoa Wa Mwanza Mhe John Mongela, Naibu waziri Wa Wizara ya ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe Angelina Mabula ambaye pia ni Mbunge Wa Jimbo la Ilemela, Maaskofu Wa makanisa mbalimbali nchini sambamba na Mbunge Wa Jimbo la Singida Magharibi Mhe Elibariki Kingu.
MWISHO.
No comments:
Post a Comment