Naibu Waziri wa Madini Mhe Doto Mashaka Biteko akizungumza na Uongozi wa Wilaya ya Kahama Mkoani Shinyanga ambapo amesisitiza viongozi kusimamia Kanuni na taratibu juu ya usimamizi wa madini, leo 3 Februari 2018. Picha Zote Na Mathias Canal
Kamati ya
ulinzi na usalama Wilaya ya Kahama ikiongozwa na Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe Fadhil
Nkulu wakisikiliza maelekezo mbalimbali kutoka kwa Naibu Waziri wa Madini Mhe
Doto Mashaka Biteko alipozuru Wilayani humo kwa ziara ya kikazi, Leo Februari 2018.
Mgeni Rasmi-Naibu Waziri wa Madini Mhe Doto Mashaka Biteko akizungumza wakati wa kikao cha kazi na Uongozi wa Wilaya ya Kahama Mkoani Shinyanga aakiwa katika ziara ya kikazi, leo 3 Februari 2018.
Na Mathias Canal, Shinyanga
"Sheria mpya ya madini ya mwaka 2017 inataka kurudisha
uchumi wa madini kuwa uchumi fungamanishi kwa sekta nyingine, Hatuwezi kuwa na
Mgodi ndani ya nchi ambao ajira zote zinapelekwa nje ya nchi kupitia huduma
mbalimbali, unaweza kuagiza bidhaa za kila aina kutoka nje ya nchi lakini
huwezi kuagiza ajira za wananchi wako zitoke nje kuja ndani, kamwe
haiwezekani"
Ni Kauli ya Naibu Waziri wa Madini Mhe Doto Mashaka Biteko leo 3
Februari 2018 wakati akizungumza na Uongozi wa Wilaya ya Kahama Mkoani
Shinyanga ambapo amesisitiza zaidi viongozi wa serikali katika maeneo yao
kusimamia Kanuni na taratibu juu ya usimamizi wa madini.
Mhe Biteko alikaririwa akisema kuwa usimamizi madhubuti wa
sheria na taratibu zilizowekwa ni sehemu imara na makini itakayowanufaisha
watanzania ambapo watakuwa wamemuunga mkono kwa vitendo Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Pombe Magufuli ambaye amejidhatiti kwa
mtazamo wa kuwanufaisha watanzania kupitia rasilimali zao.
Kanuni
ya madini ya mwaka 2018 imeelekeza kuwa mgodi wowote unapoanza asilimia 100% za
watoa huduma za chakula wanapaswa kuwa watu wa wananchi wa Tanzania, Pia huduma
za ulinzi kwa asilimia 100% zinapaswa kutolewa na kampuni za ndani. Hivyo
wataalamu wa sekta ya madini ni lazima kusimamia Kanuni hizo kwa usahihi.
Mhe Biteko aliongeza kuwa kampuni ya kigeni inaweza kufanya
huduma hizo lakini ni lazima iingie ubia na wananchi wa Tanzania na kanuni hizi
serikali imeziweka kwa makusudi kabisa ikiwa na mtazamo wa kuwanufaisha
wananchi kupitia rasilimali zao.
Mhe Biteko alisema kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ndicho
kimeingia mkataba na wananchi katika kuwatumikia kwa usimamizi madhubuti
kupitia ilani ya uchaguzi ya mwaka 2015-2020 hivyo viongozi wa CCM wanapaswa
kusimamia vyema serikali ili kuongeza tija katika utendaji.
Sambamba na CCM kusimamia vyema serikali pia Naibu Waziri huyo
wa Madini amewataka watendaji wote wa serikali kuwa na umoja katika utendaji
wao kwa usimamizi madhubuti wa rasilimali madini huku akitoa onyo Kali kwa
watendaji wa serikali, Viongozi, vyama vya siasa na wananchi kujihusisha na
rushwa kwani kufanya hivyo ni kuzififisha juhudi za serikali ya awamu ya Tano
inayoongozwa na Rais Magufuli ya kuwainua wananchi wanyonge ili kila mtanzania
aweze kunufaika na rasilimali zilizopo.
"Ndugu zangu ni aibu mno dhahabu na madini yetu mengine
kuchimbwa nchini lakini yanajenga nchi nyingine, Uhakika wa barabara bado
hatuna katika maeneo mengi, maji bado hatuna, sekta ya afya haijaimarika,
Zahanati zina shida lakini pia Karibu kila maeneo hatujajidhatiti kwa asilimia
100% Kwa hiyo Mhe Dc naomba sana msicheke na mtu yeyote anayecheza na
rasilimali zetu This Must be a Serious business, Mimi najua we have the same
spirit lazima tufanye kazi kwa weledi.
Aidha, Naibu Waziri huyo wa Madini Mhe Doto Mashaka Biteko
amempongeza Mkuu wa Wilaya ya Kahama Mhe Fadhil Nkulu sambamba na Mbunge wa
Jimbo la Msalala Mhe Ezekiel Maige kwa jukumu kubwa la utendaji wao katika
kuimarisha juhudi na ufanyaji kazi uliotukuka katika sekta ya madini kwa
maslahi ya wananchi na Taifa kwa ujumla huku akisisitiza kuwa kila kiongozi
atapimwa kwa matokeo ya utendaji kazi wake na si kwa cheo chake.
" Waheshimiwa Viongozi, Mhe. Rais na wanatanzania
watatupima kwa matokeo si kwa nafasi na vyeo vyetu" alisisitiza Mheshimiwa
Biteko wakati akihitimisha hotuba yake kwa uongozi wa serikali wilayani Kahama.
MWISHO.
No comments:
Post a Comment