Mbunge wa Jimbo la Ilemela ambae pia ni Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe Dkt Angeline Mabula amewataka wananchi kuwa wazalendo kwa kuwafichua wasio raia wa Tanzania katika zoezi la uandikishaji vitambulisho vya Taifa.
Mhe Dkt Angeline Mabula ameyasema hayo alipofanya ziara ya kushtukiza katika kituo cha uandikishaji wa vitambulisho vya taifa (NIDA) kilichopo ofisi ya kata ya Ibungilo ambapo amewaasa wananchi waliokuwa wamepanga foleni kwaajili ya zoezi hilo kuwa makini na waangalifu katika ujazaji wa fomu za maombi sanjari na kuwaripoti wale wote wasiostahili wakitaka kutumia mwanya huo kujipatia vitambulisho hivyo huku akiwaelimisha juu ya umuhimu wa kuwa na kitambulisho hicho
‘… Lazima muwe makini mnapojaza taarifa zenu lakini lingine sisi ni wa Tanzania tunatakiwa kuwa wazalendo kama unajirani yako ambaye si Mtanzania na amepanga foleni kutaka kupata kitambulisho cha taifa toa taarifa mapema, Tusiwape watu wasiohusika ni nyinyi wakuisaidia Serikali vinginevyo vitambulisho vyetu vitachukuliwa na watu wasiokuwa waTanzania …’ Alisema
Kwa upande wake msimamizi wa mamlaka ya vitambulisho vya taifa (NIDA) kata ya Ibungilo Ndugu Eric Elisha mbali na kueleza juu ya mwenendo wa zoezi hilo kwa kata anayoisimamia amemuhakikishia mbunge huyo umakini na uzingatiaji wa haki kuhakikisha kila mwananchi anayestahili anapata kitambulisho
Nao wananchi waliojitokeza katika zoezi la uandikishaji wamemshukuru Mhe Mbunge kwa kufanya ziara hiyo ya kushtukiza kukagua mwenendo wa zoezi huku wakiwasilisha changamoto wanazokutana nazo na kumuomba kuwasaidia namna ya kuzipatia ufumbuzi
Ziara hiyo ya gafla pia ilihusisha kulitembelea na kuzungumza na wafanya biashara wa soko kuu la wilaya hiyo la Kiloleli kujua changamoto wanazokutana nazo ili kuzipatia ufumbuzi huku akiwaasa wale wote wanaofanya biashara nje ya soko kurudi sokoni hapo kwani nafasi bado zipo zakutosha
‘ Ilemela ni yetu, tushirikiane kuijenga’
Imetolewa na
Ofisi ya Mbunge
Jimbo la Ilemela
14.01.2018
No comments:
Post a Comment