Thursday, December 28, 2017

WAZIRI MKUU AKAGUA UJENZI WA ZAHANATI MIBURE

 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Mkuu wa Mkoa wa Lindi Godfrey Zambi, alipowasili kwenye uwanja wa ndege wa Nachingwea, kwa ajili ya mapumziko ya mwisho wa mwaka ambapo aliamua kukagua miradi ya maendeleo jimboni kwake wilayani Ruangwa, mkoani Lindi, Desemba 28, 2017. (Picha Zote na Ofisi ya Waziri Mkuu)
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na mwananchi wa kijiji cha Mibure, Mzee Menrad Kilian, baada ya kukagua ujenzi wa zahanati kijijini hapo, wilayani Ruangwa mkoani Lindi, Desemba 28, 2017. 
 Waziri Mkuu,Kassim Majaliwa akizungumza na wananchi wa kijiji cha Mibure, wakati alipoenda kukagua ujenzi wa zahanati ya kijiji hicho Desemba 28, 2017. Waziri Mkuu yupo jimboni kwake kwa mapumziko ya mwisho wa mwaka
Mkurugenzi Mtendaji wa KALIF Construction, Ally Mohamed Libaba akitoa maelezo kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa (katikati) wakati wakijaribu kuvuta maji kutoka kwenye pampu ya mradi wa maji wa kijiji cha Namakuku, Desemba 28, 2017. Wa kwanza kulia ni msimamizi wa mradi huo, Bw. Fadhil Ally Libaba. 

*Aagiza zahanati ikiisha ipelekewe kifaa ca kutunzia watoto njiti

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameanza ziara fupi ya siku tatu, kukagua miradi ya maendeleo jimboni kwake katika wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi.

Waziri Mkuu ambaye yuko kwenye mapumziko ya mwisho wa mwaka, amekagua miradi ya maji, ujenzi wa zahanati na kuzungumza na wananchi kaika vijiji vya Mibure, Namakuku, Chienjere, Namahema A na Namahema B.

Akizungumza na wakazi wa kijiji cha Mibure jana mchana (Alhamisi, Desemba 28, 2017) mara baada ya kukagua zahanati ya kijiji hicho, Waziri Mkuu alisema ameridhishwa na ujenzi unavyoendelea na akamwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ruangwa ahakikishe zahanati hiyo ikikamilika inapata kifaa cha kuwatunzia watoto njiti kwa sababu kijiji hicho kiko mbali na Hospitali ya Wilaya ya Ruangwa.

“Nilileta makontena yenye vifaa vya hospitali, na humo ndani mlikuwa na vifaa vya kuwatunza watoto njiti (watoto wanaozaliwa kabla ya muda kutimia). Hakikisha hawa wanapata kifaa hicho kwa sababu hawana gari la kubeba wagonjwa, na pia wako mbali na hospitali ya wilaya na pia kituo cha afya cha jirani kiko mbali pia,” alisisitiza.

Akizingumzia kuhusu upatikanaji wa umeme kijiji hapo, Waziri Mkuu alisema: “Mibure ipo kwenye mipango ya kupata umeme ambao unatoka Nagurukuru, -Nghimbwa-Chienjere-Namakuku-Mibure.”

Aliwataka vijana wa kata hiyo, wachangamkie fursa kwa muanda mitaji ya kuwa na gereji za kuchomelea vyuma, saluni na viwanda vidogo vya usindikaji.

Mapema, akisoma taarifa ya ujenzi wa zahanati ya Mibure mbele ya Waziri Mkuu, Mwenyeiti wa kijiji hicho, Bw. Samwel Chilemba alisema mradi huo umekwishagharimu sh. milioni 52, ambapo kazi zilizokamiliak ni jengo la zahanati, kichomea taka na choo chenye matundu matatu.

Alisema wanakabiliwa na changamoto ya kupanda holela kwa gharama za vifaa vya ujenzi, kupokea michango kidogo kutoka kwa wananchi, ukosefu wa nyumba ya mganga na wauguzi na kiasi cha fedha cha sh. milioni 8.26 za kununulia samani.

Bw. Chilemba alisema kukamilika kwa ujenzi wa zahanati hiyo kutasaidia wakazi wa vijiji jirani vya Njawale, Namakuku, na vijiji jirani vya wilaya ya Nachingwea ambavyo vinapakana na wilaya ya Ruangwa.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
ALHAMISI, DESEMBA 28, 2017

No comments:

Post a Comment