Na Mwashungi Tahir,Maelezo Zanzibar
VIJANA wa Chama cha Mapinduzi Zanzibar, wametakiwa kujiepusha na tabia ya majungu na makundi ambayo yanaweza kuhatarisha uhai wa chama.
Akizungumza katika mapokezi ya uongozi mpya wa Umoja wa Vijana Taifa wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM), Mwenyekiti wa wa Umoja Kheir Denis James katika makao makuu Gymkhana mjini Zanzibar, alisema panapo makundi ni vigumu kustawisha chama.
Aliwahimiza vijana wa chama hicho kufanya kazi kwa kuzingatia maadili, katiba na kanuni zilizopo sambamba na kuzidisha ushirikiano.
Mwenyekiti huyo aliyechaguliwa hivi karibuni katika mkutano mkuu wa CCM uliokwenda sambamba na chaguzi za jumuiya zake mbalimbali, alisema vijana ndio msingi unaotegemewa katika kukiimarisha chama hicho hasa katika siasa za ushindani wa vyama vingi.
“Lazima sisi vijana tutambue wajibu wetu, chama kinatutegemea ili kukiimarisha na kuwa mfano wa uongozi bora unaofuata misingi ya kidemokrasia pamoja na kuhimili vishindo vya upinzani,” alisema James.
Kwa upande mwengine, amewataka Wenyeviti na Makatibu wa Mikoa na Wilaya waendane na kasi ya serikali ya awamu ya tano chini ya uongozi wa Rais Dk. John Pombe Magufuli, na kuongza kuwa asiyekuwa tayari kwa hilo ni vyema akae pembeni ili awapishe wawezao kuendelea na majukumu.
Aliwataka vijana wawe wahangaikaji, wapambanaji na kutotishwa na baadhi ya watu wenye vyeo vikubwa, kwani kila mtendaji anapaswa kuheshimu nafasi ya mwenzake pahali pa kazi.
Aidha aliwahakikishia vijana kuwa atalishughulikia jengo lao kwa kuliimarisha pamoja na kusimamia miradi yote ya maendeleo waliyoanzisha sasa na baade ili kuwa na jumuiya imara.
Alihitimisha kwa kuwakumbusha Wabunge na Wawakilishi wanaojisahau na kutopita majimboni baada ya kuchaguliwa, waelewe kwamba wanabeba dhima kubwa kwa kuwanyima wapiga kura wao haki ya kutumikiwa.
Mapema, Makamu Mwenyekiti wa UVCCM Bi. Taifa Maulid Mwita, amewataka vijana kujitambua na kuwa wasikivu akisema nidhamu ndio kila kitu katika kuendeleza jumuiya yao.
Aidha amewataka kuongeza ushirikiano kwani kufanya kazi kwa pamoja ndiko kutakokiletea tija chama hasa katika kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu wa tafa mwaka 2010.
Ameusifia uongozi wa Dk. John Magufuli uliojikita katika kupambana na rushwa, uhujumu uchumi na wizi wa rasilimali za taifa kwa staili yake ya ‘Hapa kazi tu’ ambayo imeanza kurejesha heshima ya taifa.
Aidha aliipongeza Serikali ya Mapinduzi Zanzibar chini ya uongozi thabiti wa Rais Dk. Ali Mohamed Shein, kwa namna inavyofanya kazi na kuinua maisha ya wazee, wanawake na vijana.
Viongozi hao waliwasili Zanzibar jana Disemba 27, 2017 na kupata mapokezi makubwa wakitokea mjini Dodoma ambako walichaguliwa kwa kupata kura nyingi katika uchaguzi wa UVCCM.
IMETOLEWA NA IDARA YA HABARI MAELEZO.
No comments:
Post a Comment