Naibu Waziri wa Maliasili na
Utalii, Japhet Hasunga ( mbele ) akiwa
na baadhi ya viongozi wa Hifadhi za Taifa
pamoja kamati ya ulinzi na
usalama kutoka Wilayani Bagamoyo akiongoza kwenda kuangalia sehemu
kunakofanyika utalii wa boti katika
Hifadhi ya Taifa ya Saadani wakati Naibu Waziri huyo alipotembelea
hifadhi hiyo jana kwa ajili ya kujionea changamoto mbalimbali zinazoikabili .
Wananchi wa Kitongoji
cha Uvinje kilichomo ndani Hifadhi
ya Taifa ya Saadani iliyopo wilayani Bagamoyo Mkoani wa Pwani wamesema hawapo tayari kuhama wala kulipwa fidia ili kupisha hifadhi hiyo.
Kitongoji
hicho, ambacho ni kati ya vitongoji nane vya Kijiji cha Saadani, kilitakiwa
kiondolewe tangu mwaka 2005 baada ya hifadhi hiyo kupandishwa daraja kutoka
pori la akiba na kuwa hifadhi kwa mujibu wa Tangazo la Serikali Namba 281 la
Septemba 16, 2005.
Akizungumza
mbele ya kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya
ya Bagamoyo, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga wakati alipofanya ziara jana katika kijiji hicho aliwambia wananchi hao kuwa lengo
la ziara yake ni kutaka kuwasikiliza juu mgogoro huo na sio kuwahamisha.
‘Mimi
ni mgeni kidogo kwenye Wizara hii, Nimekuja kuangalia sio kuwahamisha kwa kuwa sijui eneo hili lina
ukubwa kiasi na lina kaya ngapi lakini
nimekuja kutembelea hifadhi na maeneo yote yenye changamoto. ‘’ alisema
Alisema amefika kwa ajili ya kuwasikiliza ili aweze kujua jinsi mgogoro
ulivyo kwa sababu hakutaka kusikia
upande mmoja wa TANAPA pekee.
Naye , Kaimu Mwenyekiti wa Kitongoji hicho, Hassan Akida alisema wakazi wa eneo hilo hawapo tayari kuhama na
wala kulipwa fidia kwa vile ni ardhi yao
tokea enzi za mababu zao.’
‘Tumesema hapa ndo kwetu mnataka
kutuhamisha mtupeleke wapi wakati sisi tumezoea maisha yetu hapa’’ alisema
Akida.
Aliongeza
kuwa kitongoji hicho kimekuwapo kwa muda mrefu na waliishi bila
shida hadi pale pori hilo lilipobadilishwa na kuwa Hifadhi ya
Taifa
“Wakati hili ni pori la akiba tuliishi
vizuri tu na wazazi wetu walikuwa ni wafanyakazi wa pori. Lakini tangu iwe
hifadhi imekuwa taabu. Sasa tunafukuzwa wakati
tumezaliwa hapa na wazazi wetu wamezikwa hapa hapa,” anasema Hassan Akida.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Kijiji cha Saadani, Adam Mwandosi
alisema mgogoro huo umedumu kwa
muda mrefu na umekuwa ukileta chuki kati
ya Serikali na wananchi.
Amesema
wananchi wa eneo hilo muda mwingine wamekuwa wakimuona hata yeye Mwenyekiti wao kama anawasaliti kwa vile tokea mgogoro huo ulipoanza viongozi wengi wamekuwa wakifika hapo lakini
wamekuwa hawana majibu ya kumaliza mgogoro huo.
Mhifadhi Mkuu wa Saadani, Stepahano Msumi
amesisitiza kuwa kitongoji hicho kimo ndani ya hifadhi kinyume cha sheria.
Alisisitiza
kuwa sheria za hifadhi za Taifa haziruhusu makazi ya watu ndani yake.
“Kwa
ufupi tu ukiangalia GN (Tangazo la Serikali) linaonyesha kuwa eneo lote la
kitongoji cha Uvinje liko ndani ya hifadhi. Ni kweli lilikuwa eneo la watu
ambao walikuwa watumishi wa pori la akiba tangu lilipoanzishwa mwaka 1968.
Waliombwa kuondoka lakini waliendelea kuongezeka,” anasema.
Anasema
katika makubaliano, iliamuliwa kuwa walipwe fidia kwa taratibu lakini hata hivyo licha ya kutekeleza utaratibu wa fidia
bado wamegoma kuipokea mbali ya wachache kujitokeza.
Ikumbukwe
kuwa, Saadani ni hifadhi pekee ya Taifa nchini na Afrika Mashariki yenye fukwe
za bahari na inayotazamana na Bahari ya Hindi na fukwe zake zinakutana na uoto
wa asili wa nchi kavu.
Inapatikana
katika mikoa ya Tanga na Pwani. Uwepo wake ni matokeo ya pori la akiba la
Saadani, ranchi ya Mkwaja na sehemu ya kaskazini, sambamba na akiba ya msitu wa
asili wa Zaraninge.
No comments:
Post a Comment