WAZIRI MKUU
Kassim Majaliwa amempa mwezi mmoja Ofisa Ardhi wa wilaya ya Namtumbo Bw. Maurus
Yera awe ametafuta ardhi ya kuwafidia wakazi wa kijiji cha Lwinga wilayani Namtumbo.
Wakazi hao 21
mwaka 2008 eneo lao lenye ukubwa wa ekari 101 lilitwaliwa na Serikali kupitia
halmashauri ya wilaya hiyo kwa ajili ya kupisha ujenzi wa shule ya sekondari ya
mkoa wa Ruvuma na waliahidiwa kulipwa fidia.
Waziri Mkuu
alitoa agizo hilo jana jioni (Alhamisi, Novemba 23, 2017) alipozungumza na
wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa michezo wa
Lwinga akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Ruvuma.
Alitoa agizo
hilo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi hao kupitia mabango,
ambapo walimuomba awatatulie kero hiyo ya madai ya fidia ya ardhi iliyodumu kwa
miaka 10 bila kupatiwa ufumbuzi.
Waziri Mkuu
alisema haoni sababu ya Halmashauri hiyo kushindwa kuwafidia wananchi hao
sehemu ya ardhi kwa muda wote huo ukizingatia wilaya hiyo ina hifadhi ya ardhi.
“Nataka
wananchi hawa wawe wamelipwa fidia yao ya ardhi kabla ya siku kuu ya Krismasi
ya mwaka huu. Serikali haiko tayari kuona wananchi wake waliotoa ardhi kupisha
maendeleo wakisumbuliwa.”
Waziri Mkuu
alisema Serikali ya awamu ya Tano chini ya Rais Dkt. John Magufuli inataka kila
mtumishi ahakikishe anatumia taaluma yake vizuri kwa kuwahudumia wananchi ikiwa
ni pamoja na kutatua kero zinazowakabili kwa wakati.
Pia Waziri
Mkuu alitoa wito kwa wananchi hao kuhakikisha hawakubali kutoa rushwa pale
wanapohitaji kupata huduma mbalimbali kutoka kwa watumishi kwa kuwa ni haki yao
kuhudumiwa.
Aliwataka
wananchi kuwa na imani na Serikali yao na kuiunga mkono katika mapambano dhidi
ya rushwa kwani vitendo hivyo vinakwamisha shughuli za maendeleo ya wananchi na
Taifa kwa ujumla.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewataka watendaji
kuhakikisha miradi wanayosimamia inakuwa na thamani inayolingana na kiasi cha
fedha kilichotolewa na iwapo watabainika kwenda kinyume hatua kali
zitachukuliwa dhidi yao.
“Lazima kiasi
cha fedha kinachotolewa kugharamia mradhi kilingane na thamani ya mradi husika.
Mfano tumetoa sh. milioni 70 kugharamia mradi na kukuta mradi uliojendwa ni wa sh.
milioni 30 aliyeshughulikia ujenzi huo nasi tutamshughulikia hatutamuacha salama.”
Awali, Waziri Mkuu alifungua ghala la kuhifadhiia mpunga na
mchele katika wilaya ya Namtumbo lililojengwa na MIVARF na kisha alizungumza na
watumishi wa halmashauri hiyo na kuwataka wafanye kazi kwa bidii na kuzingatia
maadili ya utumishi wa umma.
Kwa upande
wake Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Bibi Christine Mndeme alisema mkoa huo unakabiliwa
na changamoto mbalimbali ikiwemo ya ukosefu wa masoko kwa mazao ya mahindi na
mbaazi, ambapo Waziri Waziri Mkuu alisema sula hilo linashughulikiwa hivyo
wananchi waendelee kuwa na subira.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
iJUMAA, NOVEMBA 24, 2017.
No comments:
Post a Comment