Na Fatma Salum – MAELEZO
Serikali imewaagiza watendaji
wakuu na viongozi wote Serikalini kuzingatia kikamilifu mwongozo wa
maandalizi ya mpango wa bajeti ya mwaka 2018/2019 ili uweze kuleta tija
na kuendeleza mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Tano.
Agizo hilo limetolewa jana na
Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa wakati akitoa hutuba ya kuahirisha
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mjini Dodoma.
Majaliwa aliagiza kuwa watendaji
hao ambao ndio maafisa masuuli katika taasisi zao wahakikishe
wanazingatia mambo yote muhimu yaliyoainishwa kwenye mwongozo ili
kuimarisha usimamizi na utekelezaji wa mpango wa bajeti.
Alibainisha kuwa miongoni mwa
mambo ya kuzingatia ni ukusanyaji wa mapato ya ndani ambapo aliwataka
maafisa masuuli kuhakikisha makusanyo yote yanawekwa kwenye mfuko mkuu
wa Serikali.
“Maafisa masuuli waendelee
kupunguza matumizi ya Serikali kwa kufanya tathmini ya uendeshaji wa
taasisi zao ili kuchukua hatua stahiki na kuhakikisha taasisi
zinazojiendesha kibiashara zinapata faida na kuacha kutegemea ruzuku
kutoka Serikali kuu,” alisema Majaliwa.
Katika kudhibiti matumizi na
kupunguza gharama, Majaliwa aliwataka waendelee kufanya uhakiki wa
watumishi ili mishahara ilipwe kwa watumishi wanaostahili, wanaopaswa
kupandishwa madaraja wahakikiwe na malimbikizo yote ya madeni
yabainishwe ili yaweze kulipwa.
Aidha, Majaliwa aliwaagiza
maafisa masuuli hao kuhakikisha madai ya watoa huduma wote yanahakikiwa
na mkaguzi mkuu wa ndani wa hesabu za Serikali na kuingizwa kwenye
hesabu za fungu husika.
“Serikali inawataka kutoingia
mikataba ya miradi mipya bila kuwa na uhakika wa upatikanaji wa fedha
pamoja na kuzingatia matumizi ya hati za ununuzi zinazotolewa kwenye
mfumo wa malipo ili kudhibiti malimbikizo ya madai,” alisisitiza
Majaliwa.
Nao wakurugenzi wa halmashauri
zote nchini wametakiwa kuzingatia miongozo inayotolewa na kuwashirikisha
wananchi pamoja na wadau wa sekta binafsi katika kupanga mipango ya
maendeleo kwenye maeneo yao.
Pia Majaliwa aliagiza Wizara ya
Fedha na Mipango kukamilisha kazi ya kuandaa mwongozo wa maandalizi ya
mpango wa bajeti na kuusambaza kwa wadau wote ili taasisi zote za umma
zianze mchakato wa maandalizi ya bajeti ya mwaka 2018/2019.
No comments:
Post a Comment