Mkurugenzi wa Shughuli za
Kitakwimu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Irenius Ruyobya akizungumza
na waandishi wa habari (hawapo pichani) hivi karibuni kuhusu
maadhimisho ya Siku ya Takwimu Afrika yatakayofanyika kesho tarehe 20
Novemba, 2017 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Mwalimu Julius
Nyerere jijini Dar es Salaam.
…………………………………………………………..
Na: Veronica Kazimoto-Dar es Salaam,
Maadhimisho ya Siku ya Takwimu
Afrika yatafanyika kesho tarehe 20 Novemba, 2017 katika Kituo cha
Mikutano cha Kimataifa cha Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa
habari jijini Dar es Salaam hivi karibuni, Mkurugenzi wa Shughuli za
Kitakwimu kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Irenius Ruyobya alisema
maadhimisho hayo yanayoratibiwa na ofisi hiyo kwa niaba ya Serikali,
yana lengo la kuongeza ufahamu kuhusu nafasi na mchango wa Tasnia ya
Takwimu katika kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii Barani Afrika.
Ruyobya alisema kuwa kaulimbiu ya Siku ya Takwimu Afrika kwa mwaka huu ni “Takwimu Bora za Uchumi kwa Maisha Bora”
“Kaulimbiu hii inalenga kuweka
mkazo katika matumizi ya Takwimu za Uchumi kwa ajili ya kuboresha maisha
ya wananchi wote nchini na Afrika kwa ujumla”, amebainisha Ruyobya.
Ruyobya alifafanua kuwa matumizi
sahihi ya Takwimu za Uchumi yanaiwezesha Serikali kutunga sera na
kutathmini programu mbalimbali kama vile Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa
Miaka Mitano (FYDP-II), Agenda ya Dunia ya Mwaka 2030 ya Malengo ya
Maendeleo Endelevu (SDGs) na Agenda ya Afrika ya Mwaka 2063.
“Progaramu zote hizi, zina lengo
la kuboresha maisha ya wananchi kwa kuhakikisha kuwa, kuna upatikanaji
wa Huduma za afya, Elimu, Miundombinu ya umeme na barabara, Mawasiliano,
Utunzaji wa mazingira pamoja na Utawala bora”, amesema Ruyobya.
Jumla ya washiriki 200 kutoka
katika Wizara, Idara na Taasisi za Serikali, Wadau wa Maendeleo, Vyuo
vya Elimu ya Juu, Wanafunzi wa Shule za Sekondari pamoja na Wadau
mbalimbali wa takwimu nchini wanatarajiwa kuhudhuria kwenye maadhimisho
hayo.
Siku ya Takwimu Afrika
huadhimishwa kila mwaka tarehe 18 Novemba ambapo kwa mwaka huu, Tanzania
itaadhimisha siku hiyo kesho tarehe 20 Novemba, 2017.
No comments:
Post a Comment