Na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Dodoma
Mkuu
wa Mkoa wa Dodoma Mheshimiwa Dkt. Binilith Mahenge amewataka watumishi wa Umma
na Taasisi mbalimbali kwenye Mkoa wa Dodoma kuhakikisha wanatimiza majukumu yao
ya utekelezaji wa shughuli za maendeleo na kuwahudumia Wananchi kikamilifu na
kwa uadilifu wakitambua kuwa sasa Mkoa wa Dodoma ndio Makao Makuu ya Nchi.
Aidha
amesema yapo baadhi ya maeneo Mkoa bado haufanyi vizuri hususani katika sekta
ya elimu ambapo hali ya ufaulu hairidhishi.
Akiwa
wilayani Mpwapwa katika ziara yake ya kutembelea wilaya za Mkoa wa Dodoma kwa
lengo la kujitambulisha Dkt. Mahenge amesema eneo la Elimu ya Msingi na
Sekondari hali ya ufaulu hairidhishi ambapo Mkoa umeshika nafasi ya 24 kati ya
Mikoa 26 kwenye matokeo ya Mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwaka
2017, Wakati kwa upande wa Matokeo ya Mtihani wa kumaliza elimu ya Sekondari
kidato cha nne mwaka 2016 Mkoa ulikuwa wa 19 kati ya Mikoa 26.
Amesema
viongozi hao wanayodhamana kubwa kwa Wanadodoma kwenye masuala yote ya
maendeleo kama vile Elimu, Afya, Kilimo, Uwekezaji, Viwanda na Biashara na
kutumia fursa ya kuwa jirani na Serikali katika kusukuma mbele masuala ya
Maendeleo kwenye Mkoa.
Amewataka
Viongozi na Watendaji wote kwenye Wilaya za Mkoa wa Dodoma kutambua wana jukumu
kubwa la kusimamia elimu kwenye Wilaya zao na ameagiza kila Wilaya ikae na
kufanya tathimini ya sababu ya kufanya vibaya kwenye matokeo ya mitihani ya
msingi na sekondari na kutafuta majibu ya changamoto hizo na pia kubuni
mikakati itakayo ukwamua Mkoa kielimu na baadae mipango hiyo ya Wilaya
ijadiliwe pamoja ili kutoka na mkakati mmoja wa Mkoa wa kupandisha hali
ya Elimu na Ufaulu kwenye Mkoa wa Dodoma.
Dkt.
Mahenge amezitaka Wilaya za Mkoa wa Dodoma kujipanga vizuri kwenye Sekta ya
kilimo akiainisha kuwa Viongozi na Watendaji kwenye Mkoa wana jukumu la
kuhakikisha tatizo la upungufu wa chakula linakuwa historia kwenye Mkoa wa
Dodoma kwa kuhimiza Wananchi wetu kulima mazao yenye kustawi hata katika
mazingira ya maji kidogo na hali ya hewa ya Mkoa wa Dodoma kama Mtama, Uwele,
Muhogo na Alizeti.
Aidha,
Katika kukuza mapato na uchumi wa Halmashauri za Mkoa wa Dodoma, Dkt. Mahenge
amezitaka Halmashauri hizo kwa sasa kuanza uwekezaji kwenye kilimo cha Korosho
ambacho kimewasaidia wakulima wengi kuinua hali ya uchumi kwenye maeneo
wanayolima zao hilo.
Amesema
tayari wataalamu wa kilimo wamebainisha kuwa zao hilo linauwezo wa kustawi
vizuri na kuwa na mavuno ya kuridhisha kwenye Mkoa wa Dodoma na kiuchumi soko
la Korosho lipo na bei ya zao hilo kwenye soko ni nzuri. Ameipongeza Wilaya ya
mpwapwa kwa jitihada walizoanza za kuwekeza kwenye kilimo cha Korosho na
amezitaka Wilaya nyingine Mkoani Dodoma kuona namna nazo zinavyoweza kuanza
utekelezaji wa mpango huo wa kilimo cha Korosho.
Dkt.
Mahenge amezitaka Wilaya za Mkoa wa Dodoma kuweka mkakati wa utekelezaji wa
Kampeni ya Serikali ya Uanzishaji wa Viwanda kwa kila Mkoa uliozinduliwa hivi
karibuni na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Mheshimiwa Seleman Jafo kwa
kuzishirikisha hadi ngazi za chini kwenye wilaya zetu na kutaka mkakati huo
ulenge kuanzisha viwanda vinavyozalisha bidhaa zinazotokana na malighafi ya
mazao yanayolimwa kwenye Mkoa wa Dodoma.
Aidha,
ametaka Mkakati huo wa uanzishaji Viwanda kwa kila Wilaya uwajumuishe Vijana na
Wanawake, kwa kuwaagiza Wakurugenzi wote wa Halmashauri za Wilaya Mkoani
Dodoma kuhakikisha wanatenga asilimia kumi (10%) kwenye bajeti zao za
Halmashauri kwa ajili ya miradi ya uzalishaji mali na uchumi kwa vijana na
wanawake, na fedha hizo zipelekwe kwenye kuanzisha viwanda vidogovidogo kwa
ajili ya makundi hayo.
Dkt.
Mahenge amebainisha kuwa tayari amekutana na kuzungumza na makundi mbalimbali
kwenye Mkoa yakiwemo ya Wazee, Viongozi wa Madhehebu ya Dini, Wafanyabiashara
na Wakuu wa Vyuo Vikuu na Elimu ya Juu ambapo amekutana na Malalamiko ya baadhi
ya watumishi kutokuwa waadilifu na kutotekeleza wajibu wao ipasavyo wa
kuwahudumia wananchi.
Kwa
upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Jabir Shekimweri amemwelezea Dkt.
Mahenge kuwa bado Makusanyo ya Wilaya hiyo hayaridhishi kwani kwa mwaka wa
fedha 2016/2017 Wilaya ya Mpwapwa ililenga kukusanya zaidi ya shilingi
2,800,000,000 lakini mapato halisi yalikuwa Shilingi takribani Bilioni moja, akibainisha
kuwa hali hiyo inatokana na uchache wa vyanzo vya mapato hivyo ili kukuza
mapato na hali ya uchumi tayari Wilaya ya Mpwapwa imeanza utekelezaji wa
Mkakati wa kukuza kilimo cha Korosho.
“Kwa
kushirikiana na Bodi ya Korosho tayari Wilaya ya Mpwapwa tumepokea jumla ya
tani sita (6) za mbegu bora na za muda mfupi za Korosho na pia tumefikia
makubaliano na Bodi ya Korosho ya kujenga kiwanda cha kubangua
Korosho hapa Mpwapwa jambo ambalo litakuza sana kilimo cha korosho na kuingizia
Wananchi na Wilaya kwa ujumla pato kubwa na kukuza uchumi” amebainisha
Mheshimiwa Shekimweri.
Mheshimiwa
Shekimweri amesema tayari Wilaya ya Mpwapwa imeanza kuitikia Maelekezo ya
Serikali ya kuanzisha Viwanda na tayari Wilaya imetenga eneo la hekta 3.7
kwa ajili ya uanzishaji wa viwanda ambapo baada ya upimaji wa eneo hilo jumla
ya viwanja 40 vilipatikana kwa ajili ya ujenzi wa viwanda.
Pamoja
na kuzungumza na watumishi wa Serikali Wilayani humo, Mkuu wa Mkoa Dkt. Mahenge
alitembelea kitalu cha miche ya Korosho kwenye Gereza la Mpwapwa,alitembelea
kituo cha utafiti wa Mifugo Mpwapwa, Mradi wa kiwanda cha kukamua alizeti
na kujibu kero za wananchi kwenye mkutano wa hadhara kijiji cha Chitemo.
MWISHO
No comments:
Post a Comment