Mbunge
wa Muleba Kusini (CCM), Prof. Anna Tibaijuka, ametangaza kung’atuka
nafasi ya ubunge kwa kutogombea tena kwenye uchaguzi mkuu ujao wa mwaka
2020.
Prof.
Tibaijuka alitangaza msimamo huo jana mkoani Kagera, wakati
wakizungumzia miaka miwili ya serikali ya Rais John Magufuli ambaye hivi
sasa yuko mkoani humo kwa ziara za kikazi.
Jumatatu
ya wiki iliyopita, Lazaro Nyalandu, ambaye alikuwa Mbunge wa Jimbo la
Singida Kaskazini kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), alitangaza
kujiuzulu ubunge na pia kujivua uanachama wa CCM kutokana na kile
alichoeleza kuwa ni kutoridhishwa na mwenendo wa chama hicho.
Baadaye
Nyalandu alionekana akikaribishwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema). Kisheria, kuhama chama humpotezea mbunge sifa ya kuendelea
kuwa mwakilishi wa jimbo lake na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) huandaa
uchaguzi mwingine mdogo kwa ajili ya kumpata mbunge mwingine kwenye
jimbo husika.
Wakati
akifafanua kuhusu uamuzi wake wa kutogombea tena ubunge mwaka 2020,
Tibaijuka aliyewahi kuwa Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi,
aliiambia Televisheni ya Taifa (TBC), kuwa ameamua kujing’atua ili kutoa
nafasi kwa vijana.
“Sisi
ni watu wazima… kizazi chetu tumeshamaliza kazi. Tumeshastaafu na mimi
nikimaliza ubunge muhula huu nastaafu, nakwenda Muleba,” alisema
Tibaijuka na kuongeza:
“Na
kuaga nimeshaaga na wananchi wameniamini. Napenda tuwape nafasi vijana.
Kuzeeka haimaanishi kwamba maarifa yangu yaondoke kwa sababu
nimestaafu, tunawapa nafasi vijana washike nchi.
“Baba
wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere alisema tung’atuke… na mimi nang’atuka
ili maarifa yetu yaweze kutumika kushauri, jamani tufanye hivi ili
tuende mbele.”
Akizungumzia
utendaji wa serikali ya Rais Magufuli katika kipindi cha miaka miwili
tangu aingie madarakani Novemba 5, 2015, Tibaijuka alisema amefanya
mengi mazuri na lazima Watanzania waendelee kumuamini.
“Hii
nchi ilikuwa inasubiri kiongozi si Rais. Rais lazima awe pia kiongozi…
sasa tujifunze kujua tofauti, mtu anaweza kukalia nafasi, lakini
anaongoza? Anaonyesha njia? Ni jasiri? Kwa maana ujasiri unatokana na
ukweli,” alisema.
Tibaijuka
aliondolewa katika nafasi ya uwaziri kwenye serikali ya awamu ya nne ya
Rais (mstaafu) Jakaya Kikwete wakati baadhi ya wabunge walipomhusisha
na kashfa ya uchotwaji wa mabilioni ya shilingi kwenye Akaunti ya Tegeta
Escrow iliyokuwa Benki Kuu (BoT).
No comments:
Post a Comment