Saturday, November 11, 2017

MHANDISI MTIGUMWE AITAKA BODI YA KAHAWA KUONGEZA UZALISHAJI

Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Mhandisi Mathew Mtigumwe akikagua kiwanda kidogo cha uzalishaji wa kahawa katika Bodi ya Kahawa mara baada ya kuwasili Ofisi hizo kwa ziara ya kikazi.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Mhandisi Mathew Mtigumwe akikagua namna Kahawa inavyohifadhiwa tayari kwa kuingia sokoni.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Mhandisi Mathew Mtigumwe akisikiliza maelezo ya kitaalamu kuhusu mchakato mzima wa kupaki kahawa na soko lake kutoka kwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu/Mkurugenzi wa Ubora wa kahawa na uhamasishaji masoko Ndg Primus Kimaryo.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Mhandisi Mathew Mtigumwe alipotembelea chumba cha kuchotea Sampuli zinazopelekwa ambazo ni kilo 8 na kuchotea Gramu 300 kwa Loti.
Muonjaji katika Maabara ya Kahawa Bi Regina Mushi Daud akiendelea na majukumu yake katika maabara ya Kahawa.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu/Mkurugenzi wa Ubora wa kahawa na uhamasishaji masoko Ndg Primus Kimaryo Kutoka Bodi ya Kahawa akielezea mbele ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Mhandisi Mathew Mtigumwe namna wanunuzi wanavyokabiliana katika ununuzi wa Kahawa
Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Mhandisi Mathew Mtigumwe akizungumza na wafanyakazi wa Bodi ya Kahawa mara baada ya kuwasili kwa ziara ya kikazo
Baadhi ya wafanyakazi wa Bodi ya Kahawa wakifatilia kikao kilichoongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Mhandisi Mathew Mtigumwe katika Ukumbi wa Bodi hiyo.
Picha ya pamoja wafanyakazi wa Bodi ya Kahawa pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Mhandisi Mathew Mtigumwe.

Na Mathias Canal, Kilimanjaro

Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Mhandisi Mathew Mtigumwe ameitaka Bodi ya Kahawa ambayo ni Taasisi ya serikali iliyopewa jukumu la kusimamia sekta ya Kahawa nchini kuongeza ufanisi katika uzalishaji wa Kahawa nchini kwani  Kahawa ni miongoni mwa mazao ya kipaumbele.

Mhandisi Mtigumwe ametoa Rai hiyo wakati akizungumza na Wafanyakazi wa Bodi ya Kahawa Mara baada ya kutembelea Ofisi za Bodi hiyo zilizopo Mtaa wa Railway, Kata ya Mawenzi Katika Manispaa ya Moshi Mkoani Kilimanjaro.

Alisema kuwa Mwaka 2011 wadau waliandaa na kupitisha mkakati wa miaka 10 wa maendeleo ya Kahawa ambayo lengo kuu ilikuwa ni kuongeza uzalishaji hadi kufikia Tani 80,000 Mwaka 2017 na Tani 100,000 Mwaka 2021 lengo ambalo halijafikia na bado uzalishaji ni mdogo hivyo kuongeza uzalishaji linapaswa kuwa jambo la haraka iwezekanavyo.

Katibu Mkuu Alimuelekeza Kaimu Mkurugenzi Mkuu/Mkurugenzi wa Ubora wa Kahawa na uhamasishaji Masoko Primus Kimaryo Kufanya Utafiti ili kubaini nini chanzo cha uzalishaji mdogo wa Kahawa iwapo wananchi kutotunza vizuri kahawa yao, Hali ya hewa na udongo au mbegu sio nzuri zinazotumika.

Aliongeza kwa kusema kuwa Serikali inajipanga kwa kampeni kubwa kutoa elimu kwa wananchi juu ya kufahamu umuhimu wa kulima kwa wingi mazao ya Chakula na Biashara ikiwemo zao la Kahawa.

Hata hivyo Katibu Mkuu huyo, Alisema miongoni mwa sababu ambazo huchangia uzalishaji mdogo katika mazao mbalimbali nchini huwa ni pamoja na Wananchi kuchanganya mazao wakati wa kupanda jambo ambalo sio rafiki sana katika Kilimo, sambamba na Kutoacha nafasi kati ya mche na mche.

Mhandisi Mtigumwe aliitaka Bodi ya Kahawa Kufanya Utafiti wa maeneo ambayo Kahawa inastawi kwa wingi ili kuongeza sehemu za kuzalisha Kahawa kufikia uzalishaji wa kiwango kikubwa tofauti na ilivyo hivi sasa.

Hata hivyo amesema kuwa atazishughulikia haraka iwezekanavyo Changamoto za Uzalishaji, Changamoto za Ubora, Changamoto za Masoko sambamba na Changamoto za Sekta.

Majukumu ya Bodi ya Kahawa ni pamoja na usimamizi wa sheria namba 23 ya marekebisho yake ya Mwaka 2009 na kanuni za Kahawa 2013 sambamba na kuratibu Majukumu shirikishi (Shared Functions) Baina ya serikali na wadau.

MWISHO

No comments:

Post a Comment