Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Njombe NEEMA MGAYA (Katikati
Mstari wa Mbele) akiwa na baadhi ya wanawake aliowakabidhi vyerehani 370 vyenye
thamani zaidi ya Shilingi Milioni 90 Halmashauri ya Makambako Mkoani Njombe ili
wajikwamue kiuchumi.
Baadhi ya vyerehani 370 vyenye thamani zaidi ya Shilingi Milioni
90 vilivyolewa na Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Njombe NEEMA MGAYA vikiwa
tayari kukabidhiwa kwa baadhi ya wanawake wa Mkoa wa Njombe ili wajikwamue
kiuchumi.
Na
Mwandishi Wetu, Makambako Njombe
Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Njombe NEEMA MGAYA ametoa
msaada wa vyerehani 370 vyenye thamani zaidi ya Milioni 90 kwa wanawake mkoani
humo ili wajikwamue kiuchumi huku akiunga mkono juhudi za Serikali inayohimiza
uchumi wa viwanda.
Akizungumza Mjini Makambako wakati wa hafla ya kukabidhi
vyerehani hivyo kwa baadhi ya wanawake, MGAYA amesema amefikia uamuzi huo ili
kuunga mkono juhudi za Rais DK John Pombe Magufuli kuifanya Tanzania kuwa taifa
la uchumi wa kati kupitia viwanda.
Akibainisha zaidi ameeleza juhudi za kumkomboa mwanamke
wa mkoa wa Njombe ni jambo linalopiganiwa kwa miaka mingi hivyo vyerehani hivyo
vitawafungulia njia kuweza kujikwamua kiuchumi.
“Nimekuwa sina papara katika utendaji wangu, mwaka jana
nilitoa msaada wa vitabu vya ziada kwa Shule za Sekondari Halmashauri ya Makambako,
ambapo kwa mwaka huu nimeamua kuunga mkono juhudi za serikali upande wa viwanda
kwa kuwasadia wanawake hawa vyerehani hivi 370,” alisema Mgaya.
Akifafanua amesema anatambua thamani kubwa walionayo
wanawake hivyo kwa kuwawezesha vyerehani hivyo kutainua familia na jamii zinazowazunguka
kwani fedha zitakazopatikana zitasaidia huduma za kijamii na mahitaji mengine.
“Mtu ninayemthamini huwa nampa kitu ambacho kitadumu na
kumsaidia kwa muda mrefu, mimi nimeamua kutowapa samaki kwani mtamla ataisha,
nimewapa nyavu ambayo mtaitumia kuvua samaki, nendeni mkavitunze vyerehani hivi
kujiletea maendeleo endelevu,” alisema Mgaya.
Akizungumza baada ya kupokea cherehani yake Diwani wa
Viti Maalum Lupembe Neema Limbanga amesema alilolifanya Mbunge huyo wa Viti
Maalum halijawahi kutokea katika maisha yake na kwamba vyerehani hivyo vimewafungulia
njia kimaisha.
Naye Diwani wa Viti Maalum CCM Njombe STELLA FRANCIS amesema Mgaya
amewapa zawadi ambayo licha ya kuwainua kiuchumi itakuwa mkombozi hasa katika
ndoa zao, kwani sasa wataweza kuhudumia familia kwa kushirikiana na wanaume
zao.
Kutolewa kwa vyerehani hivyo 370 ambavyo ni sawa na
viwanda vidogo 92 kwa dhana ya vyerehani vinne sawa na kiwanda kimoja kidogo
kunaufanya mkoa wa Njombe kuitikia vilivyo wito wa Rais DK JOHN POMBE
MAGUFULI
kuhamasisha uchumi wa viwanda.
Lengo la Mkoa kupitia wanawake ni kuwa na viwanda vidogo
35 hivyo kwa vyerehani 370 ambavyo Neema
amevitoa ni kwamba lengo la kimkoa kupitia wanawake limeshafikiwa.
No comments:
Post a Comment