Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na
Serikali(Tamisemi), Selemani Jafo amefanya ziara leo wilayani Kiteto mkoani
Manyara na kumuagiza Meneja wa Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini(Tarura)
kuhakikisha ifikapo Novemba 17 mwaka huu utekelezaji wa barabara ya Namelock yenye
urefu wa kilomita 81 uwe wa kuridhisha.
Jafo amefikia hatua hiyo baada ya kukagua barabara
hiyo na kutoridhishwa na utekelezaji wake wakati ni miongoni mwa barabara za
kimkakati za wilaya hiyo.
Amesema kama utekelezaji huo utakuwa wa kusuasua
hadi tarehe hiyo na Meneja huyo akashindwa kumchukulia hatua mkandarasi wa
ujenzi wa barabara hiyo basi ataondolewa katika nafasi hiyo meneja huyo.
“Serikali imetoa zaidi ya Sh.Bilioni 6 kwa ajili ya
ujenzi wa barabara hii lakini utekelezaji wake unasuasua nikwambie tu Meneja
nikija tena Novemba 17 nikakuta hali hii na wewe ukawa hujamchukulia hatua
mkandarasi basi nitakunyofoa wewe,”amesema Jafo
Mbali na hilo, Jafo alikagua kituo cha Afya
Engusero na kuwaahidi kuwa serikali itaendelea kuboresha huduma za afya kwenye
eneo hilo ili wananchi waweze kupata huduma bora.
“Tutaleta fedha za kujenga chumba cha upasuaji,
chumba cha kuhifadhia maiti, wodi ya kinamama na watoto pia, nimeshuhudia
changamoto zilizopo tunawahakikishia wananchi serikali ya awamu ya tano
imedhamiria kuhakikisha zinatolewa huduma bora za afya,”amesema.
Kadhalika, Jafo ametembelea shule ya sekondari
Engusero na kuzungumza na walimu na wanafunzi ambapo amewaahidi serikali
itaboresha miundombinu ya shule hiyo ili kuhakikisha wanasoma katika mazingira
mazuri.
Mara baada ya ziara hiyo, Jafo amezungumza na
wananchi wa Engusero katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye eneo hilo
ambapo amezungumzia dhamira ya serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dk.John
Magufuli katika kulinda rasilimali za Taifa hasa madini kuwa imesaidia
kuongezeka kwa mgao kwenye madini ambapo awali Tanzania ilikuwa haipati.
Amesema serikali inaendelea kutatua changamoto
mbalimbali zinazowakabili wananchi na kuwataka kufanya kazi kwa bidii na kuanzisha
kwa viwanda vya usindikaji mazao ikiwemo alizeti.
Kwa upande wake, Mbunge wa Kiteto Emmanuel Papian
ameishukuru serikali kwa kuendelea kutatua changamoto zinazowakabili wananchi
wake huku akiomba serikali kuwapatia fedha za ujenzi wa uzio katika shule ya
sekondari Engusero ili kuwalinda wanafunzi.
Aidha amesema wilaya hiyo inakabiliwa na changamoto
ya ukosefu wa watumishi mbalimbali ikiwemo madaktari na kuiomba serikali
kutupia jicho na kushughulikia changamoto hizo.
No comments:
Post a Comment