Friday, November 17, 2017

DODOMA, SINGIDA KUTUMIA KILIMO CHA UMWAGILIAJI IFIKAPO 2019

Kiongozi wa msafara wa wawakilishi wa kampuni ya Henan Juren Crane Group kutoka Jimbo la Henan nchini China, Wang Yuheng (wa pili kulia) akisisitiza jambo wakati alipokutana na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Ushirika wa Shirikisho la Vyama vya Ushirika Tanzania (TFC), Bw. Henry Mwatwinza Mwimbe (kulia). Tukio hili lilifanyika jana, Alhamisi, Novemba 16, 2017 jijini Dar es Salaam.

Na Daniel Mbega
WANANCHI wa mikoa ya Dodoma, Singida, Tabora, Shinyanga na Simiyu wanaweza kujikwamua kiuchumi kwa kutumia kilimo cha umwagiliaji ifikapo mwaka 2019 kutokana na kuwepo kwa mpango wa uwekezaji unaolenga kuchimbia visima virefu pamoja na mabwawa katika maeneo mbalimbali nchini Tanzania.

Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Ushirika wa Shirikisho la Vyama vya Ushirika Tanzania (TFC Ltd), Bw. Henry Mwantwinza Mwimbe, amesema hayo jana baada ya kukutana na wawakilishi wa kampuni ya Henan Juren Group ya China, ambayo imeonyesha nia ya kuwekeza kwa ubia nchini kwa kutengeneza zana mbalimbali za kilimo ikiwa ni pamoja na kuchimba visima katika maeneo yaliyo kame.
Lengo la uwekezaji huo, kwa mujibu wa Mwimbe, ni kuwakwamua wakulima kiuchumi kwa kuwa na kilimo endelevu cha umwagiliaji badala ya kutegemea mvua, ambazo zimekuwa hazina uhakika kwa sababu ya mabadiliko ya tabianchi yanayotokana na uharibifu wa mazingira.
“Wanachama wetu karibu asilimia 80 wanajihusisha na kilimo, hivyo tunaona itakuwa ni vyema kama tutabadilisha namna ya uendeshaji wa kilimo hiki ili kilete tija kwao na kwa taifa kwa ujumla.
“Katika maeneo mengi mvua zinanyesha mara moja kwa mwaka na wakati mwingine siyo za kutosha, matokeo yake wananchi wanashindwa hata kupata mavuno yanayojidhi matumizi ya nyumbani, achilia mbali ziada ya kuuza sokoni, lakini kilimo cha umwagiliaji kina uhakika na kinaweza kuendeshwa wakati wote wa mwaka,” alieleza Mwimbe.
Alisema kwamba bado wapo katika hatua za awali kuhusu mchakato huo na akafafanua kwamba, mradi huo utawahusisha wanachama wote nchini walio kwenye ushirika ambao watashirikishwa.
Hata hivyo, alisema mradi mama ni kuunganisha (assembling) zana za kilimo kutoka China kama matrekta na mashine nyingine zinazoendana na kilimo watakazoziuza kwa wakulima wa ndani pamoja na nchi jirani, lakini wanaona kwamba hilo litafanikiwa ikiwa wakulima watajengewa uwezo hasa kwa kuwa na uhakika wa maji ili kuendesha kilimo cha umwagiliaji.
Mkalimani, Dkt. Chikira Ismail Msangi, akifasili kuhusu azma ya wawekezaji hao katika kuanzisha kampuni ya ubia itakayounganisha zana za kilimo kama matrekta na mitambo ya uchimbaji visima na umwagiliaji hapa nchini. Kulia ni Mkurugenzi wa Maendeleo ya Ushirika wa Shirikisho la Vyama vya Ushirika Tanzania (TFC), Bw. Henry Mwimbe. Tukio hili lilifanyika jana, Alhamisi, Novemba 16, 2017 jijini Dar es Salaam.
“Vijijini watu wana matrekta lakini yanatumika mara moja tu kwa mwaka kwa sababu ya kutegemea mvua, kwa kutumia kilimo cha umwagiliaji ni wazi kwamba wakulima watahitaji nyenzo zaidi ili kurahisisha kilimo chao, lakini lazima kwanza maji yapatikane.
“Israel ni nchi ya jangwa, lakini leo ukienda imebadilika kutokana na kuwepo kwa visima vilivyochimbwa pamoja na mabwawa na wanalima mazao mengi yenye ubora na kuyasafirisha duniani kote, sisi Tanzania tunayo ardhi ya kutosha ambayo tunashindwa kuitumia kwa kuwa tu mahali pengi hakuna vyanzo vya uhakika vya maji.
“Shinyanga, Simiyu, Tabora, Singida, Dodoma na Manyara ni mikoa ambayo ina shida kubwa ya maji japo ina ardhi kubwa, lakini kama watachimbiwa visima wanaweza kufanya kilimo kwa uhakika na kuwavutia hata vijana wanaokimbilia mijini kutafuta ajira,” alisema.
Mwimbe alisema kwamba, katika maeneo ambayo yana mito na vijito kama ya mikoa ya Mtwara, Lindi, Ruvuma, Rukwa, Katavi na mingineyo, wanaweza kuchimbiwa mabwawa makubwa ya kuvuna maji ya mvua ambayo yatatumika kwenye kilimo cha umwagiliaji wakati wa kiangazi.

Wachina wako tayari
Hii ni mitambo itakayounganishwa hapa nchini ambayo ni maalum kwa shughuli za ujenzi na uchimbaji wa mabwawa ya maji.
Bw. Henry Mwimbe (kulia) Mkurugenzi wa Maendeleo ya Ushirika wa TFC akionyesha kufurahishwa na picha za mitambo ya uchimbaji mabwawa. Tukio hili lilifanyika jana, Alhamisi, Novemba 16, 2017 jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Maendeleo ya Ushirika wa TFC, Bw. Henry Mwimbe (kulia), alitazama zana na mitambo mbalimbali ambayo itaunganishwa hapa nchini katika uwekezaji wa pamoja baina ya TFC na kampuni ya Henan Juren Cranes Group kutoka China. Tukio hili lilifanyika jana, Alhamisi, Novemba 16, 2017 jijini Dar es Salaam.
Uchunguzi wa MaendeleoVijijini unaonyesha kwamba, wawekezaji hao kutoka China wako tayari kwa mradi huo na kwamba wanaweza kukaa chini na TFC kuangalia namna gani utakavyoendeshwa.
Mmoja wa wawakilishi hao, Wang Yuheng, alisema lengo kubwa ni kuleta teknolojia ya wakulima wa chini ili kuinua kilimo chao kilete tija na ikiwezekana wazalishe bidhaa wanazoweza kuzisafirisha nje ya nchi.
“Tunataka kuja kuwaletea teknolojia wakulima wa hali ya chini, tunajua zana za kilimo zinaweza kurahisisha kilimo chao, lakini tutazungumza na TFC ili kuona vipaumbele vyao vingine katika kilimo ni nini, mbali ya upatikanaji wa maji,” alisema Wang.
Wang alisema kwamba, zana zote hizo zitakuja kuunganishwa hapa hapa Tanzania badala ya kuziingiza zikiwa tayari, hali ambayo itasaidia pia taifa kuingiza fedha za kigeni pamoja na kutoa ajira kwa vijana wa Tanzania pamoja na kujifunza ujuzi mbalimbali.
Maofisa wengine walioongozana na Wang ni Si Yongbin, Si Guanlei na Zhai Qinwu ambao kila mmoja ni mtaalam wa teknolojia mbalimbali.

Watembelea EPZA
Wawakilishi hao wa kampuni ya Henan Juren Group, jana walitembelea Mamlaka ya Maeneo Maalum ya Uwekezaji (EPZA) jijini Dar es Salaam ambapo walionyesha kuridhishwa kwa kiwango kikubwa na maelezo waliyopewa kuhusu fursa za uwekezaji zilizopo nchini.
Mkuu wa Mawasiliano ya Umma wa EPZA, Nyanda Shuli, aliwatoa mashaka kwamba hakuna urasimu wowote kwa wawekezaji, wawe wa ndani au wa nje, na kuwahakikishia kwamba mazingira ya uwekezaji nchini Tanzania ni rafiki.
“Tunayo maeneo mengi ya uwekezaji hapa nchini na kilimo kinapewa kipaumbele kikubwa kwa sababu ndicho kinachozalisha malighafi za viwanda, ardhi inayofaa kwa kilimo imetumika kwa asilimia 35 tu, hivyo bado kama taifa tunahitaji kuwekeza zaidi ili tuzalishe bidhaa za kuuza nje,” alisema Nyanda.
Mkurugenzi wa Maendeleo ya Ushirika wa TFC, Henry Mwimbe (wa pili kushoto) akijadiliana jambo na baadhi ya wadau katika makao makuu ya Mamlaka ya Maeneo Maalum ya Uwekezaji Tanzania (EPZA) jijini Dar es Salaam jana, Alhamisi, Novemba 16, 2017.
Bw. Nyanda Shuli (wa pili kulia mwenye miwani), Mkuu wa Mawasiliano ya Umma wa Mamlaka ya Maeneo Maalum ya Uwekezaji Tanzania (EPZA), akifafanua jambo kwa Mkurugenzi wa Maendeleo ya Ushirika wa TFC, Bw. Henry Mwimbe (wa tatu kushoto) pamoja na ujumbe wa kampuni ya Henan Juren Cranes Group kutoka China walipotembelea makao makuu ya EPZA jana Alhamisi, Novemba 16, 2017.
Bw. Nyanda Shuli akifafanua jambo katika mkutano huo.
Mkurugenzi wa Maendeleo ya Ushirika wa TFC, Bw. Henry Mwimbe (kulia) na ujumbe wa wawekezaji kutoka China wakimsikiliza kwa makini Bw. Nyanda Shuli wa EPZA (hayupo pichani).
Ofisa Mwandamizi wa Promosheni wa EPZA, Bi. Nakadongo Fares (kulia) akisisitiza jambo kwa ujumbe wa wawekezaji kutoka China na viongozi wa Shirikisho la Vyama vya Ushirika Tanzania (TFC) wakati walipotembelea makao makuu ya EPZA, Ubungo External, jijini Dar es Salaam, jana Alhamisi, Novemba 16, 2017.
Nyanda aliongeza kwamba, kuna maeneo ya kutosha kwa uwekezaji huko Bagamoyo ambayo yako chini ya EPZA hasa kutokana na ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo itakayokuwa mkombozi kwa Watanzania kiuchumi.
“Pale zitakuja meli kubwa na mizigo, lakini tunataka zikipakua mizigo hiyo ziondoke na mizigo mingine kutoka hapa, kama Watanzania watakuwa wamezalisha bidhaa hata zitokanazo na mazao ya kilimo itakuwa fursa kubwa kupeleka nje,” alisema.
Kwa upande wake, Ofisa Mkuu wa Promosheni, Bi. Nakadongo Fares, alisema kuna unafuu mkubwa kwa wawekezaji kutoka nje wanaopitia EPZA kuliko kama wakija wenyewe moja kwa moja, kwani mamlaka hiyo inayo maeneo tayari yaliyotengwa kwa ajili ya uwekezaji wa kila aina.
“Uunganishaji wa matrekta unafanyika hapa pamoja na viwanda vya kuongeza thamani ya mazao ambayo yanasafirishwa nje kwa ubora wa hali ya juu, tunashauri hata mitambo na zana zenu mje mziunganishie hapa hapa ili kutoa na ujuzi kwa Watanzania,” alisema Bi. Fares.

Kuhusu Henan Juren Group
Kampuni ya Henan Juren Crane Group ipo katika Mtaa wa Weizhuang Industrial Park, katika kitongoji cha Changyuan, jijini Xinxiang katika Jimbo la Henan katika Bara China, na inaongozwa na Bw. Jason Zhang.
Kampuni hiyo, ambayo awali ilijulikana kama Henan Juren Crane Co., Ltd, ilianzishwa mwaka 1987 ikijihusisha zaidi na utengenezaji wa crane, lakini sasa inazo kampuni tanzu kama Henan Juren Crane Services Co., Ltd., Henan Juren Advertisement Co., Ltd. na Hexin Machinery & Electronic Co., Ltd ambayo inajihusisha zaidi na utengenezaji na zana mbalimbali zikiwemo za kilimo na umeme. 
Kampuni hiyo ina mtaji wa Yuan za Kichina RMB120,000,000 (takriban Dola za Kimarekani 18,108,561.60), na rasilimali zenye thamani ya Yuan 200,000,000 (sawa na Dola 30,180,936.00) ambapo inazo karakana tatu katika wilaya ya kusini, wilaya ya kaskazini na wilaya mpya huku ikimiliki eneo lenye ukubwa wa meta za mraba 460,000 na wafanyakazi zaidi ya 1,200.
Kwa mujibu wa rekodi za mwaka 2001, uchunguzi unaonyesha kwamba, mapato yalikuwa kati ya Dola 2.5 milioni na Dola 5 milioni.
Hizi ni crane na madaraja maalum yanayoundwa na kampuni ya Henan Juren Cranes Group inayotaka kuwekeza nchini.
Makao makuu ya kampuni ya Henan Juren Cranes Group katika Jiji la Xinxiang katika Jimbo la Henan nchini China.

No comments:

Post a Comment