Friday, October 20, 2017

WAZIRI WA MAJI ATEMBELEA MRADI WA LONGIDO

1Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Isack Kamwelwe akikagua chanzo cha maji cha Mto Simba, wilayani Siha.
2Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Isack Kamwelwe akiangalia kazi ya uunganishaji wa mabomba yanayolazwa kwa ajili ya mradi wa Longido, Siha, mkoani Kilimanjaro.
3Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Isack Kamwelwe na Mkurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira (AUWSA), Mhandisi Ruth Koya Kilimanjaro, wakiwa mbele ya tenki la maji Longido.
4Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Isack Kamwelwe akizungumza na wakazi wa Kijiji cha Engikaret, ambao ni miongoni mwa watakaonufaika na mradi wa maji wa Longido, mkoani Arusha.
……………
Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Isack Kamwelwe ametembelea Mradi wa Maji Longido, mkoani Arusha kufuatilia maendeleo ya utekelezaji wake, kwa lengo la kuhakikisha unakamilika kwa wakati na kumaliza kero ya maji kwa wakazi wa Longido.

Mhandisi Kamwelwe ametembelea mradi huo na kuridhishwa na hatua iliyofikiwa hadi sasa, ambao Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliweka jiwe la msingi mnamo Oktoba 21, 2017 na kuagiza ukamilike kwa wakati na kuanza kuhudumia wakazi wa Mji wa Longido na Kijiji cha Engikaret.

‘‘Serikali imedhamiria kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa majisafi na salama Wilayani Longido kwa kutekeleza mradi huu mkubwa wa maji kutoka katika chanzo cha maji cha Mto Simba kilichopo Wilaya ya Siha, mkoani Kilimanjaro umbali wa kilomita 64 mpaka Longido.’’

‘‘Nimeridhishwa na hatua ya utekelezaji wa mradi huu unaosimamiwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira ya Mji wa Arusha (AUWSA) na utaigharimu Serikali kiasi cha Sh. bilioni 15.8 ambazo ni fedha za ndani’’, alisema Waziri Kamwelwe.

Mradi huo unategemea kuzalisha lita 2,160,000 kwa siku wakati mahitaji halisi kwa sasa ni lita 1,462,000, na unatarajiwa kuongeza upatikanaji wa maji kwa asilimia 100 (sawa na wakazi 26,145 kwa sasa) wa Mji wa Longido  kufikia 2024 na Kijiji cha Engikaret chenye wakazi wapatao 1,294.

No comments:

Post a Comment