WAZIRI
wa Nchi Ofisi ya Rais (TAMISEMI), Seleman Jafo amewataka Wakuu wa Mikoa nchini
kuhakikisha kuwa kila mmoja anajenga viwanda vipya 100 kuanzia Desemba 2017
hadi Desemba 2018.
Akizungumza na Wakuu wa
mikoa wapya walioapishwa leo Ikulu Jijini Dar es Salaam, na kufanya nao
mazungumzo katika Ofisi ya TAMISEMI Jijini Dar es Salaam, Waziri Jafo alisema
lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa ifikapo Desemba 2018, mikoa yote 26 ya
Tanzania Bara inakuwa na viwanda vipya 2600.
Waziri Jafo alisema Serikali
ya Awamu ya Tano imekusudia kufikia nchi ya uchumi wa kipato cha kati kupitia
ujenzi wa viwanda, hivyo aliwataka wakuu wa Mikoa yote nchini kuhakikisha kuwa
wanaibua viwanda vidogo na vya kati kwa kuhamasisha ushiriki wa Viongozi ndani
ya mikoa na wananchi wote katika maeneo yao ya utawala.
Aliongeza kuwa katika
kusimamia utekelezaji wa agizo hilo, Ofisi yake itaweka utaratibu maalum wa
kupima utendaji kazi wa Kila Kiongozi wa Mkoa katika kuangalia ushiriki wake wa
kuwajengea hamasa Viongozi wa chini wakiwemo Wakuu wa W ilaya na wananchi.
“Serikali itatoa
vyeti kwa Mikoa yote itakayofanya vizuri katika ujenzi wa viwanda, hatua hii
inalenga kutoa motisha kwa mikoa iliyobaki kuweza kujifunza na kubaini mbinu
mbadala katika kuibua viwanda ili kuweza kuwakomboa kiuchumi wananchi” alisema
Jafo.
Kwa mujibu wa Waziri
Jafo alisema katika kufanikisha dhana ya ujenzi wa uchumi wa viwanda nchini Serikali
inaendelea kuweka mkazo na kipaumbele katika upatikanaji wa malighafi za kilimo,
na hivyo kuwataka Wakuu wa Mikoa kuhakikisha kuwa Maafisa Ugani wanatekeleza
vyema majukumu yao ya kazi.
Aidha Jafo aliwataka
Wakuu wa Mikoa nchini kusimamia vyema makusanyo ya fedha za ndani
zinazokusanywa katika Halmashauri zote nchini na kutumia vyema fedha za asilimia 5 zilizotengwa katika halmashauri
kuwawezesha na kuhamasisha wananchi kupata mikopo ili kuwawezesha kushiriki katika
ujenzi wa uchumi wa viwanda.
Waziri Jafo pia aliwataka
Wakuu wa Mikoa kuwaelekeza Maafisa
Maendeleo ya Jamii nchini kuweza kuhamasisha wananchi kujiunga katika vikundi vya
ushirika ili weweze kupatiwa mikopo kupitia mifuko ya fedha inayotolewa na Serikali
na hivyo kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa uchumi.
Kwa upande wake, Mkuu
wa Mkoa wa Mara Adam Malima alisema ili kufanikisha dhana ya uchumi wa viwanda,
Serikali haina budi kuwapa msukumo na ushirikiano wa karibu Wanasayansi ili kuwawezesha kuibua viwanda
vingi zaidi pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa malighafi za kilimo nchini.
MWISHO
No comments:
Post a Comment