Wananchi wasifia makubaliano serikali, Barrick
-
- Imeandikwa na Matern Kayera
-
- WANANCHI wamesema makubaliano yaliyofi kiwa kati ya Serikali na
Kampuni ya Barrick Gold ni hatua muhimu kwa taifa kuanza kunufaika na
rasilimali hiyo.
Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Methodius Kilaini
aliliambia gazeti hili jana kuwa Rais John Magufuli amethubutu kufanya
jambo kubwa, ambalo lilikuwa likiogopwa kwa muda mrefu la kuzungumzia
umuhimu wa rasilimali kuwanufaisha wazawa. Alisema hatimaye taifa
limethubutu kusema hapana na kuwataka wawekezaji hao kuingia kwenye
mazungumzo kuhusu madini hayo.
Alisema makubaliano yaliyofikiwa kati ya Serikali na Barrick ni hatua
kubwa ya kusonga mbele katika kusimamia rasilimali za nchi. “Kwa mara
ya kwanza tumefanikiwa kukutana na kuzungumza na watu ambao zamani
tulikuwa tukiwaogopa. Baadhi ya watu walimbeza Rais Magufuli kuwa eti
tutashitakiwa, tutafilisiwa lakini hatimaye leo muafaka umepatikana,”
alisema Askofu Kilaini.
Kuhusu kamati hiyo ya majadiliano iliyoongozwa na Waziri wa Katiba na
Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi, Askofu Kilaini alisema inapaswa
kupongezwa kwa kazi nzuri na uzalendo walioonesha katika kuhakikisha
kuwa mazungumzo hayo yanazaa matunda. Kwa upande wake, Mhadhiri katika
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Bashiru Ally alisema kuwa pamoja na
mafanikio yaliyopatikana katika mazungumzo hayo, Taifa linapaswa
kuendelea kutafakari zaidi kuhusu hali yake ya kiuchumi.
Dk Bashiru alisema kuwa ni jambo jema kuwa na sheria ya madini
inayoipa nguvu Serikali, Bunge na wananchi katika kusimamia rasilimali
ya madini, lakini ili taifa liondokane na udumavu wa kimaendeleo
linapaswa kuwekeza zaidi kwenye mambo yanayowezekana kwa urahisi kama
vile kilimo, ufugaji na viwanda. “Uwezo wetu wa kuwekeza kwenye sekta ya
madini ni mdogo.
Kwenye madini kunahitajika teknolojia na mtaji mambo ambayo kwa kiasi
kikubwa hatuna uwezo nayo. Vita ya uchumi bado mbichi, hatua ya Rais ya
kushughulikia matatizo hayo itupe funzo katika kutoka hapo na tujikite
zaidi kwenye kujitegemea kwa kuzalisha vitu ambavyo tuna uwezo navyo
kama vile sukari, nguo na vyakula,” alieleza Dk Bashiru.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mabenki nchini (TIOB), Patrick
Mususa alisema kuwa makubaliano hayo yanatia moyo kwa kuwa nchi ilikuwa
imeibiwa na kuonewa. Alisema hayo ni matumaini mapya kwa kuwa nchi
iliumia kutokana na kuwa na misingi mibovu, mipango mibovu na sheria
kandamizi za madini dhidi ya wananchi ambazo ziliwabeba zaidi
wawekezaji.
“Barrick imekubali kulipa zaidi Sh bilioni 700, itaisaidia Serikali
katika kutoa huduma za jamii kama ujenzi wa miundombinu, elimu na afya.
Lakini pia gawio la 50 kwa 50 ya faida itakayotokana na madini hayo pia
litainufaisha sana taifa ikilinganishwa na ilivyokuwa awali,”alisema
Mususa.
Mwenyekiti wa Kamati ya Majadiliano hayo kati ya Serikali na Barrick,
Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi alitaja malengo
ya Serikali katika majadiliano hayo na baadhi yake ni kuainisha fidia
kutokana na makosa mbalimbali yaliyofanywa na makampuni tanzu ya Barrick
nchini, kujadili na kuweka mfumo mpya wa uendeshaji wa shughuli za
uchimbaji na biashara ya madini ili kuleta mgao sawa wa mapato kati ya
Serikali na Kampuni ya Barrick.
Malengo mengine ni kujadili na kukubaliana muundo na mfumo wa
uendeshajii utakaoiwezesha Tanzania kupata manufaa zaidi kutokana na
uwekezaji unaofanywa na migodi, kubadilisha mikataba ya uendeshaji
migodi ili iendane na marekebisho ya sheria ya madini. Ikumbukwe kwamba
Rais Magufuli aliunda Tume mbili za kuchunguza biashara ya madini.
Tume ya kwanza iliongozwa na Profesa Abdulkarim Mruma iliyoanza kazi
Machi 29 hadi Mei 24 mwaka huu. Tume ya pili iliongozwa na Profesa
Nehemiah Osoro iliyoanza kazi Aprili 11 hadi Juni 12 mwaka huu na kisha
akaunda Kamati ya Majadiliano iliyoongozwa na Waziri wa Katiba na
Sheria, Prof Palagamba Kabudi ambayo iliwasilisha taarifa yake kwa Rais
jana.
No comments:
Post a Comment