NA TIGANYA VINCENT-RS-TABORA
JUMLA ya shilingi bilioni 20 zimetolewa
na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii(TASAF) kwa walengwa wa Mpango wa Kunusuru
Kaya Masikini katika Halmashhauri zote za Tabora kwa ajili kunusuru
kaya maskini katika eneo hilo.
Kauli hiyo ilitolewa jana mjini Tabora
na Mratibu wa TASAF Mkoa huo Ngoko Buka wakati wa kikao cha kutathmini
utekelezaji wa TASAF Awamu ya Tatu sehemu ya kwanza kilichowashirikisha
Wafadhili ,viongozi kutoka makao Makuu TASAF na wale wa Mkoa na Wilaya
ya Uyui.
Alisema kuwa fedha hizo zilitolewa
katika kipindi cha kuanzia Julai 2015 hadi Agosti mwaka huu ambapo jumla
ya walengwa 45,928 waliwezwa kunufaika na fedha hizo na hatimaye
kubadilisha maisha yao.
Buka alisema kuwa fedha zimesaidia
baadhi ya walengwa kuanzisha miradi mbalimbali kama ufugaji wa
kuku,bata,mbuzi ,ng’ombe ,ujenzi wa nyumba bora, kusomesha watoto,
kuwapa huduma ya kliniki na kuimarisha kilimo.
Alisema kuwa mambo mengine ambayo
walengwa wamenufaika nayo ni pamoja na uanzishaji wa biashara mbalimbali
ambayo kwa kiasi kikubwa imebadilisha maisha ya walengwa.
Naye Mkuu wa Msafara wa TASAF kutoka
Makao Makuu Dkt. Jasson Bagonza alisema kuwa wako mkoani Tabora
kuangalia utekelezaji wa miradi mbalimbali inayoratibiwa na Mfuko huo na
kujadiliana na wadau mbalimbali ili kuona kama inakwenda malengo ya
uanzishaji wake.
Alisema kuwa baada ya tathmini hiyo
watakuja na TASAF awamu ya Tatu sehemu ya pili iliyoboreshwa kwa ajili
ya maendeleo ya nchi na wananchi wake.
No comments:
Post a Comment