Wednesday, October 4, 2017

SERENGETI BREWERIES SBL YAKABIDHI MRADI WA MAJI JIMBO LA ILEMELA

Kampuni ya bia nchini ya Serengeti Breweries SBL leo imemkabidhi Mbunge wa Jimbo la Ilemela na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe Dkt Angeline Mabula mradi mkubwa wa maji wenye thamani ya shilingi Milioni 80 utakaohudumia zaidi ya wakazi 12,170 wanaoishi mitaa minne ya Kaguhwa,  Nyamadoke, Ibinza, Buyombe yote ya kata ya Nyamhongolo Jimbo la Ilemela

Akizungumza wakati wa makabidhiano ya mradi huo mgeni rasmi na mbunge wa jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula amesema kuwa kukamilika kwa mradi huo ni muendelezo wa jitihada za Serikali kwa kushirikiana na  sekta binafsi katika kumaliza changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi na kuwaletea maendeleo ikiwemo ile ya upatikanaji wa maji kupitia kampeni ya kumtua mama ndoo kichwani

‘… Huduma hii ya maji itakayopatikana hapa na tutakapoenda kuunganisha na nguvu ya Serikali maanake ni kwamba tatizo la  maji litakwenda kupungua kama si kuisha kabisa wote ni mashahidi siku tuliyoupokea Mwenge tulienda kuweka jiwe la msingi kwenye mradi mkubwa wa maji kule mlimani Nyamhongolo lakini bado kuna maeneo hayatafikiwa na mradi huu sambamba na ongezeko la watu la kila siku hivyo wenzetu Serengeti Breweries wameliona hili wameamua kutuunga mkono kama Serikali inavyosisitiza kupitia kampeni yake ya kumtua mama ndoo kichwani …’ Alisema

Mhe Dkt Angeline Mabula amezitaka kampuni mbalimbali nchini kuiga mfano wa kampuni ya bia ya Serengeti kwa kuunga mkono jitihada za Serikali katika kutatua changamoto zinazowakabili wananchi kupitia utekelezaji wa miradi yenye manufaa kwa jamii sambamba na ulipaji wa kodi

Kwa upande wake mratibu miradi wa kampuni ya bia Serengeti Breweries Limited Bi Hawa Radar amemuhakikishia mbunge huyo juu ya kampuni yake kuendelea kushirikiana na jimbo la Ilemela katika kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi wa Jimbo hilo ikiwemo hiyo ya ukosaji maji kwa muda mrefu waliyokuwa nayo wananchi wa kata ya Nyamhongolo na mitaa yake

Nae kaimu mkurugenzi wa manispaa ya Ilemela ndugu Amos Zephania amemuhakikishia Mhe Mbunge Dkt Angeline Mabula juu ya usimamizi mzuri wa mradi huo kwa kushirikiana na wananchi husika huku Mhe Diwani wa kata ya Nyamhongolo Mhe Andrea Nginila akihitimisha kwa kumshukuru na kumtaka kuendelea kumaliza changamoto nyengine zinazoikabili kata yake kwa kushirikiana

‘ Ilemela ni yetu, tushirikiane kuijenga’

Imetolewa na
Ofisi ya Mbunge
Jimbo la Ilemela
04.10.2017

No comments:

Post a Comment