Monday, October 2, 2017

RC aonya wavamizi



Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Joel Bendera
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Joel Bendera 
By Mussa Juma, Mwananchi mjuma@mwananchi.co.tz
 
Babati. Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Joel Bendera amewaonya wakazi wa mkoa huo kuvamia maeneo yaliyohifadhiwa na kuendesha vitendo vya ujangili kwani wakibainika Serikali itawachukulia hatua kali za kisheria.
Akizungumza na waandishi wa habari juzi baada ya kufunga tamasha la kupinga ujangili lililoandaliwa na Taasisi ya Chemchem Foundation katika eneo la Hifadhi ya Jamii ya Burunge, Bendera alisema wote waliovamia maeneo ya hifadhi wataondolewa.
“Kuna familia kama 17 zinaishi ndani ya eneo la Hifadhi ya Jamii Burunge, tayari wamepatiwa eneo la kwenda na tunaonya ambao watavamia maeneo ya hifadhi na kufanya ujangili kuwa watachukulia hatua kali za kisheria,” alisema.
Awali, akitoa taarifa ya utendaji, Mkurugenzi wa Chemchem Foundation, Nicolaus Negri aliwataka wananchi wanaoishi vijiji vinavyozunguka Hifadhi ya Jamii Burunge kukataa ujangili.
Negri alisema wananchi wanapaswa kukataa kununua nyama za porini kutoka kwa majangili, lakini pia wanatakiwa kutoa taarifa polisi kwa watu wanaojihusisha na biashara hiyo mitaani.
“Kama tukiacha ujangili uendelee na tukaendelea kuvamia maeneo ya hifadhi, ina maana tutakosa watalii hivyo shughuli za maendeleo zitakwama,” alisema Negri.
Taasisi ya Chemchem imewekeza kwenye hoteli katika eneo la Burunge na inamiliki kitalu cha uwindaji. Eneo hilo linapakana na hifadhi za Tarangire na Manyara ambazo hutembelewa na watalii kutoka sehemu mbalimbali duniani.

No comments:

Post a Comment