Dar es Salaam. Furaha waliyokuwa nayo baadhi ya
wakazi wa Kilimanjaro, Tanga na Dar es Salaam waliojenga pembezoni mwa
njia ya reli huenda ikageuka simanzi baada ya Kampuni Hodhi ya
Rasilimali za Reli (Rahco) kusema haina mpango wa kulegeza masharti ya
umbali wa hifadhi katika mikoa hiyo.
Awali, wakazi wa
Kilimanjaro na Tanga walifikisha vilio vyao kwa wakuu wa mikoa, ambao
walitoa maagizo ya kutumika kwa busara na mazungumzo ili kufikia muafaka
wa suala hilo, hofu yao ikiwa ni kubomolewa kwa kiasi kikubwa kwa miji
yao endapo sheria hiyo itatekelezwa.
Wananchi wengi
wanadai kuwa waliuziwa kihalali maeneo hayo na halmashauri za miji yao
na wanazo nyaraka zote za kisheria zinazoonyesha uhalali umiliki.
Septemba
29, ofisa habari wa Rahco, Catherine Moshi alisema kampuni hiyo
ilikubaliana na maombi hayo kwa kusema Tanga barabara nyingi zinakutana
na reli hivyo wakifuata sheria hasara itakuwa kubwa.
“Kuna
maendeleo mengi yamefanyika baada ya maeneo ya reli kuchukuliwa, huku
baadhi ya halmashauri zikiuza maeneo ya reli. Siyo Tanga tu, Moshi pia
tuliona tuache kutumia sheria hiyo. Hata Dar es Salaam kama tungeamua
kubomoa maeneo ya Kamata wengi wangeathirika,” alisema Moshi.
Kutokana
na hatua hiyo baadhi ya nyumba zilizokuwa zimewekea alama nyekundu ya X
zilianza kupitiwa upya na kuandikwa kwa rangi ya njano maneno
yaliyosomeka ‘Imefutwa’.
Hata hivyo, katika tangazo
lililotolewa katika gazeti hili jana, Rahco inasema bomoabomoa ya nyumba
zilizopo katika hifadhi ya reli (mita 30 kila upande) katika mikoa ya
Kilimanjaro, Tanga na Dar es Salaam iko palepale.
Tangazo
hilo lililoidhinishwa na kaimu mkurugenzi mtendaji wa Rahco linasema
kampuni hiyo itaendelea na mchakato wake wa kuwaondoa wavamizi wote wa
hifadhi za reli nchi nzima, waliopewa notisi na kuwekewa alama ya X
ikiwa ni utekelezaji wa Sheria ya Reli inayozuia ujenzi ndani ya hifadhi
njia ya reli.
“Rahco inakanusha uzushi unaoenezwa kuwa
kuna mabadiliko ya upana katika hifadhi ya reli kwa baadhi ya mikoa,”
linaeleza tangazo hilo.
No comments:
Post a Comment