Sunday, October 22, 2017

MANISPAA MPYA YA UBUNGO YAZIPIKU MANISPAA KONGWE MATOKEO DARASA LA SABA, JUHUDI ZA RC MAKONDA ZAIPAISHA DSM KITAIFA

Na Mathias Canal, Dar es salaam

HALMASHAURI mpya ya Manispaa ya Ubungo Jijini Dar es salaam inayoongozwa na Mkurugenzi Ndg John Lipesi Kayombo imetangazwa na Baraza la Mtihani Tanzania (NECTA) kuwa kinara kwa kuzipiku bila huruma baadhi ya Halamashauri zingine Kongwe nchini ambazo zimefuatia kwa mbali.

Kwa mujibu wa Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta), Dkt Charles Msonde Aliyetangaza matokeo ya mtihani wa darasa la saba Oktoba 20, 2017 Alisema watahiniwa 662,035 kati ya 909,950 waliofanya mtihani huo wamefaulu kwa kupata alama 100 au zaidi kati ya alama 250 wanazopaswa kupata.

Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo imeshika nafasi ya 11 Katika Matokeo hayo Kitaifa Kati ya Halmashauri 186 zilizopo nchini huku Mkoa wa Dar es salaam ukiongozwa Kitaifa kwa kushika nafasi ya kwanza.

Akizungumza na Mtandao wa www.wazo-huru.blogspot.com Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo Ndg John Lipesi Kayombo amesema kuwa matokeo hayo yameibua chachu ya kuongeza kasi katika uwajibikaji ambapo amewaomba maafisa elimu katika Shule za Msingi na Sekondari kutilia mkazo zaidi ili kuimarisha uelewa kwa wanafunzi na hatimaye katika Mtihani mwingine Manispaa hiyo iweze kuibuka kidedea Kitaifa.

Aliwapongeza wanafunzi wote waliofanya Mtihani na hatimaye kufanya vizuri ambapo pia amewapa heko walimu na wazazi kwa ushirikiano mkubwa katika kuongeza tija na ufaulu wa wanafunzi.

MD Kayombo Alisema kuwa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo kushika nafasi ya 11 Kitaifa sio kazi ndogo huku akizitaja Manispaa zilizopo katika Mkoa wa Dar es salaam ambazo Zina ushindani mkali kitaaluma kuwa Ni Pamoja na Ilala Mjini na Vijijini, Temeke, Kinondoni, Kigamboni na Ubungo.

Mikoa mingine iliyoongoza kitaifa ni pamoja na Dar es Salaam iliyoshika nafasi ya kwanza, Geita, Kagera, Iringa, Kilimanjaro, Njombe, Arusha, Mwanza, na Katavi.

Mkoa wa Dar es salaam Kushika nafasi ya kwanza Kitaifa katika matokeo hayo umechagizwa na Juhudi binafsi za Mkuu wa Mkoa huo Mhe Paul C. Makonda alizozianzisha za kuhakikisha Mkoa huo unaongeza ufaulu katika mitihani mbalimbali na kuwa na kuimarisha sekta ya Elimu Sambamba na sekta zingine.

Kwa mujibu wa Dkt Msonde alisema kati ya wanafunnzi waliofaulu katika matokeo hayo nchini, wasichana ni 341,020 ambao ni sawa na asilimia 70.93 na wavulana ni 321,015 sawa na asilimia 74.80 ambapo idadi ya watahiniwa waliofaulu ni sawa na asilimia 72.76.

Mwaka 2016 watahiniwa waliofaulu walikuwa asilimia 70.36, hivyo kuna ongezeko la ufaulu kwa asilimia 2.40 ambapo ufaulu katika masomo ya Kiswahili, Kiingereza na Hisabati umepanda kwa asilimia kati ya 4.25 na asilimia 10.05 kulinganishwa na mwaka 2016.

Kwa masomo ya Sayansi na maarifa ya jamii ufaulu umeshuka kwa asilimia kati ya 3.56 na asilimia 13.97 kulinganisha na mwaka 2016 ambapo shule 10 bora kitaifa ni St Peter iliyopo Kagera, St Severine  (Kagera), Alliance (Mwanza), Sir John (Tanga), Palikas  (Shinyanga), Mwanga (Kagera), Hazina (Dar es Salaam), St Anne Marie (Dar es Salaam), Rweikiza (Kagera) na Martin Luther (Dodoma).

Dkt Msonde pia alizitaja shule 10 ambazo hazikufanya vizuri kuwa ni Nyahaa ya Singida, Bosha (Tanga), Ntalasha (Tabora), Kishangazi (Tanga), Mntamba (Singida), Ikolo (Singida), Kamwala (Songwe), Kibutuka (Lindi), Mkulumuzi (Tanga) na Kitwai A (Manyara) huku mikoa iliyofanya vibaya ni Singida, Tanga, Tabora, Songwe, Lindi na Manyara.

MWISHO.

No comments:

Post a Comment