Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema
Nchimbi akikagua ukarabati wa barabara ya Malendi Wilayani Iramba yenye
urefu wa kilomita mbili ambapo ameridhishwa na ubora wa kazi hiyo. Dkt
Nchimbi amefanya ukaguzi huo kujiridhisha na ubora wa barabara zote kuu
za Kuingia na kutoka Singida katika kipindi cha mvua.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema
Nchimbi akikagua ukarabati daraja lililopo katika barabara ya Malendi
Wilayani Iramba ili kujiridhisha na ubora wa barabara zote kuu za
Kuingia na kutoka Singida katika kipindi cha mvua.
Meneja wa TANROADS Mkoa wa Singida
Mhandisi Leonard Kapongo (aliyenyoosha mkono) akifafanua jambo kwa Mkuu
wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi wakatia akikagua matengenezo ya
barabara ya Malendi Wilayani Iramba ili kujiridhisha na ubora wa
barabara zote kuu za Kuingia na kutoka Singida katika kipindi cha mvua.
Baadhi ya mafundi wakiendelea na
ujenzi wa barabara ya Malendi Wilayani Iramba yenye urefu wa kilomita
mbili ili iwe na ubora wa juu wa kupitika katika kipindi cha mvua.
……………….
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema
Nchimbi amewatoa hofu wana Singida na watanzania wote kuwa kuelekea
kipindi cha mvua barabara kuu zote za kuingia na kutoka Mkoani Singida
zinapitika vizuri.
Dkt Nchimbi ameyasema hayo mara
baada ya kukagua ukarabati wa barabara ya Malendi Wilayani Iramba ambapo
ameridhishwa na ubora wa kazi hiyo huku akimtaka Mkandarasi wa barabara
hiyo kuongea muda wa kazi ili kukamilisha matengenezo makubwa kabla ya
mvua kubwa kuanza.
Amesema barabara kuu za Kuingia na
kutoka Singida ni kiunganishi cha mikoa katika kila upande pamoja na
kuiunganisha mikoa hiyo na nchi za jirani kama Rwanda, Burundi na Kongo
ambazo hutumia barabara hizo.
Dkt Nchimbi amemtaka mkandarasi
Medics Technique Group of Company kuichukulia kwa uzito na thamani ya
kimataifa barabara ya Malendi kwa kuwa kutokamilika kwa muda
kutawaadhiri watanzania wengi na nchi za jirani kushindwa kusafirisha
bidhaa zao kwa wakati.
“Thamani ya barabara hii sio ya ki
mkoa, hapa pakiwa na shida watakaoumia sio wana Iramba au Singida
pekee, kuna magari yanasafirisha bidhaa kutoka bandarini Dar es Salaam
kuelekea nchi za jirani watapata shida pia, hivyo ni jukumu letu sote
kuhakikisha hapa panapitika kwa usalama”, amesisitiza Dkt Nchimbi.
Ameongeza kuwa kutokana na
matarajio ya Mkoa wa Singida kupata mvua za wastani na juu ya wastani
mkandarasi huyo aongeze masaa mawili kila siku ili kazi hiyo iishe
mapema na ifikapo mwezi Disemba magari yaweze kupita juu ya hiyo
barabara.
Dkt Nchimbi amemtaka mkandarasi
huyo kutengeza njia ya mchepuo yenye viwango vya juu ili barabara hiyi
ipitike wakati wowote na katika hali yoyote ile.
Aidha amezitaka halmashauri
kujiandaa kupokea mvua kwa kukagua mabwawa kama yanaweza kupokea maji ya
mvua vizuri pamoja na mifereji inayopitisha maji isafishwe mapema ili
mvua hizo zisilete madhara bali zisaidie kuifanya Singida kuwa ya Kijani
na yenye maji ya kutosha.
Amewaasa wananchi kuandaa mashamba
kwa ajili ya kilimo ili wasipishane na kipindi cha kulima, kupanda au
palizi bila kusahau kurekebisha makazi yao ili yawe imara kwa kuhimili
mvua za aina yoyote.
Kwa upande wake Meneja wa TANROADS
Mkoa wa Singida Mhandisi Leonard Kapongo amesema mradi wa Malendi
unahusisha matengenezo ya barabara yenye urefu wa kilomita mbili kwa
upande wa Singida na mita 500 kwa upande wa Mkoa wa Tabora huku
ukigharimu shilingi bilioni tatu.
Mhandisi Kapongo amesema
Mkandarasi Medics Technique Group of Company anatarajiwa kukamilisha
kazi zote mwezi Machi mwakani kwa kujenga madaraja mawili, makaravati
mawili na barabara hiyo kwa kiwango cha lami ijapokua hadi kufikia
Disemba barabara hiyo itapitika bila ya lami.
Ameongeza kuwa ana imani kuwa
mkandarasi huyo mzawa atakamilisha kazi hiyo kwa uboa unaotakiwa
kutokana na ujuzi na vifaa alivyonavyo huku akieleza kuwa kukamilika kwa
barabara hiyo kutafanya barabara zote kuu kuwa katika kiwango cha lami
yenye ubora zaidi.
Naye Diwani wa Kata ya Mgongo
Mkumbo Wilson ameishukuru serikali kwa kufanya marekebisho katika
barabara hiyo ya Malendi kwakuwa imekuwa ni eneo lenye matatizo hasa
kipindi cha mvua nyingi.
Wilson amesema kipindi cha mvua
hasa miaka miwili iliyopita maji yalikuwa yanajaa na kufunika barabara
hiyo hivyo kuhatarisha maisha ya wasafiri na wakazi wa Malendi.
Ameongeza kuwa uharibifu wa
mazingira katika mashamba yaliyo jirani na barabara hiyo yameongeza
tatizo la kujaa maji eneo hilo kwakuwa mvua zikinyesha maji yanashindwa
kuzuiwa mashambani na kujaa barabarani hivyo wataongeza bidii katika
kuelimisha jamii juu ya utunzaji wa mazingira.
No comments:
Post a Comment